WATAALAMU wa kuhakiki ubora na viwango katika shule zilizo kaunti mbalimbali nchini wanamulikwa kwa utepetevu kazini.
Maafisa hawa wanalaumiwa kwa mikasa ambayo imetokea katika taasisi za elimu.
Wanaharakati wa masuala ya elimu kutoka Homa Bay wanataka Wizara ya Elimu iwaweke kwenye mizani maafisa hawa wa uhakiki wa ubora na viwango (QASOs).
Hii ni baada baadhi ya shule hizo kuorodheshwa kuwa si salama kwa wanafunzi.
Kundi hili linadai maafisa wa elimu wanakula njama na baadhi ya shule ili kuripoti kuwa taasisi hizo ni salama licha ya kubainika kuna hatari.
Serikali iliamuru vitengo vya mabweni vifungwe kwenye shule za msingi 348 kote nchini.
Hatua hii ilichochewa na ripoti za shule kutofikia viwango vya usalama vinavyohitajiwa.
Mshirikishi wa Shirika la Elimu la Kaunti ya Homa Bay Julius Omuga alisema maafisa wa uhakiki wa ubora katika kaunti zilizoathiriwa walifeli kutekeleza majukumu yao.
Bw Omuga anaarifu maafisa hawa wanafaa kubaini matatizo hata kabla ya ripoti kutolewa.
“Ni kazi ya maafisa wa utathmini wa ubora kuhakikisha viwango vya juu vinadumishwa. Sehemu ya wajibu wao ni kuangazia usalama wa wanafunzi,” akasema.
Amri ya kufungwa kwa shule ilitolewa baada ya mkasa wa moto kukumba shule ya Hillside Endarasha Academy katika Kaunti ya Nyeri mnamo Septemba 6, 2024.
Mkasa huo ulijiri usiku wa manane na kuua wavulana 21 na kujeruhi wengine.
Hapo ndipo wizara ya elimu ikaamua kukagua shule ili kutathmini iwapo wasimamizi wamefuata viwango vya usalama kwa mujibu wa sheria.
Bw Omuga ameshikilia kuwa kusingekuwa na haja ya utathmini iwapo maafisa wa uhakiki wa viwango wangefanya kazi yao ipasavyo.
“Iwapo wangekuwa kazini, wangetambua makosa katika baadhi ya shule na kutoa mapendekezo yanayofaa,” akatilia mkazo.
Ripoti ya ukaguzi ilipendekeza kufungwa kwa shule zilizokiuka kanuni kupita kiasi.
Kulingana na Bw Omuga, shule hizi hazikufaa kufungwa.
Wizara ya Elimu inawahitaji maafisa wa kupima ubora kuhakikisha shule zina vifaa vya kuwezesha mazingira mazuri ya masomo.
Maafisa hawa wanaelekezwa kubuni na kutekeleza sera zinazohusiana na ubora pamoja na kutoa ripoti ya walichoshuhudia kwa washikadau husika.
Bw Omuga amesema maafisa hawa wanafaa kuwajibika na kutoa tahadhari mapema.
“Ina maana walifeli katika kufanya kazi ipasavyo. Hatua inafaa kuchukuliwa dhidi yao,” akasisitiza.
IMETAFSIRIWA NA LABAAN SHABAAN
Leave a Reply