Kauli ya Mhariri: Stori hii ilichapishwa mara ya kwanza katika Gazeti la Taifa Leo, la Novemba 23, 2024
RAIS William Ruto na mtangulizi wake Uhuru Kenyatta wanasemekana kuanzisha mazungumzo katika kile kinachoonekana kama jaribio la kiongozi wa taifa kupunguza uasi dhidi yake, haswa katika eneo la Mlima Kenya.
Duru zimeambia Taifa Leo kwamba, Rais Ruto pia anajaribu kuridhiana na wandani wake wa zamani ili kuongeza uthabiti katika serikali ya Kenya Kwanza.
Ushawishi wa Rais Ruto umeshuka zaidi katika Mlima Kenya kwa sababu wakazi wamekasirishwa na hatua yake ya kufanikisha kutimuliwa kwa aliyekuwa naibu rais, Bw Rigathi Gachagua.
Wakazi wa eneo hilo lililompa Rais kura nyingi katika Uchaguzi Mkuu wa 2022, pia wameelezea kutoridhishwa kwao na kutotimizwa kwa ahadi alizowapa kuelekea uchaguzi huo na uamuzi wa Dkt Ruto kufanya kazi na kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga.
Mnamo Julai mwaka huu, Rais Ruto aliwateua viongozi watano wa ODM katika baraza lake la mawaziri, hatua ambayo iliwakasirisha zaidi wakazi wa Mlima Kenya.
Kwa kuwaleta Bw Kenyatta na Bw Odinga, wanasiasa wenye uzoefu mkubwa upande wake, Rais Ruto analenga kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafuasi wao.
Baada ya kumteua Profesa Kithure Kindiki kuwa kama naibu wake, ili amsaidie katika masuala ya uongozi, duru zinasema anamfikia Bw Kenyatta ili amfaidi kisiasa haswa katika eneo la Mlima Kenya.
Dkt Ruto, Bw Kenyatta, Prof Kindiki na Bw Gachagua walishiriki jukwaa moja, katika Chuo Kikuu cha Embu wakati wa hafla ya kutazwa kwa Kasisi Peter Kimani kuwa Askofu wa Nne wa Kanisa Katoliki jimbo la Embu.
Huku Dkt Ruto, Bw Kenyatta na Prof Kindiki wakiketi pamoja na kuonyesha urafiki, Bw Gachagua alitengwa kabisa na hata kunyimwa nafasi ya kuhutubia umati.
Licha ya kwamba kambi za Dkt Ruto na Bw Kenyatta hazijatoa taarifa rasmi kuhusu mazungumzo yanayoendelea, wandani wake wanasema yapo na yanalenga kutuliza mazingira ya kisiasa.
Umoja
“Viongozi hao wawili wanazungumza chini kwa chini na hii ikaakisi wito wa Ruto kuhimiza umoja wa kitaifa katika serikali hii ya kushirikisha wote,” duru za Ikulu zikaambia Taifa Leo.
Afisa mmoja ambaye aliomba tulibane jina lake, aliongeza kuwa viongozi hao wawili walianza kuzungumza Desemba mwaka jana walipokutana Dubai.
“Mazungumzo hayo sasa yameanzishwa upya,” akaeleza.
Kando na hayo, inasemekana kuwa Rais Ruto anapanga kuwateua serikalini baadhi ya wandani wa Bw Kenyatta.
Majina ya wandani wawili wa rais huyo mstaafu yanayotajwa ni aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe na aliyekuwa Gavana wa Laikipia Ndiritu Muriithi.
“Mazungumzo kati ya rais wa nne na rais wa tano (Uhuru na Ruto) bila shaka yatakuwa ya nipe nikupe. Huku vyama vya United Democratic Alliance (UDA) haswa eneo la Mlima Kenya na chama cha Jubilee kinachoongozwa na Bw Kenyatta vinatarajiwa kupata nguvu mpya,” akasema mwandani mmoja wa Bw Kenyatta.
Akaongeza: “Haja kubwa ya Uhuru si uteuzi wa wandani wake serikalini bali ni kubuni mazingira bora kwa biashara kunawiri. Haja yake kubwa ni uchumi kuliko nyadhifa serikalini.”
Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Jeremiah Kioni aliambia “Taifa Leo” kwamba japo hana habari kuhusu mazungumzo halisi kati ya Bw Kenyatta na Rais Ruto, alisema kuwa anaongea na viongozi wengi akisaka uungwaji mkono.
“Hilo ni jambo la kawaida katika siasa; unawatafuta watu ambao unaamini wanaweza kukusaidia,” akasema Mbunge huyo wa zamani wa Ndaragua.
Leave a Reply