MADA ya ukabila imerejea katika siasa za Kenya. Katika kila mkutano wanaofanya, wanasiasa wanalaumu wengine wanaochukulia kuwa wapinzani wao kwa kuwa na nia ya kugawanya nchi kwa misingi ya kikabila.
Mada hii imeshika kasi chini ya inayoitwa Serikali Jumuishi. Kinaya ni kuwa wale wanaojifanya kulaani ukabila ndio wanaouendeleza hasa kupitia matamshi na hata vitendo vyao. Kwa kusisitiza mada hiyo katika mikutano ya kisiasa huku faraghani wakihubiri chuki za kijamii ni kuwasha moto na kuuficha chini ya nyasi kavu.
Injili hii yao inaonekana kuharibu umoja ambao vijana walionyesha walipoandamana dhidi ya Serikali Julai mwaka huu. Vijana hao waliungana bila kujali mipaka ya jamii kukosoa serikali kwa kile walichohisi ni hulka ya kutojali ya Serikali na viongozi.
Japo kumekuwa na madai kwamba maandamano hayo yalifadhiliwa na baadhi ya watu wakiwa na nia mbaya, ni wazi kuwa umoja wa vijana hao uliwashtua viongozi wa kisiasa nchini ambao wanaonekana kusuka mkakati wa kujenga taswira ya ukabila nchini wakielekeza lawama kwa wanaochukulia kuwa mahasimu na washindani wao.
Kwa kufanya hivi, wanaeneza zaidi uovu huo wanaojifanya kuupinga vita. Habari njema ni kwamba Wakenya wanaona njama yao na wanaikataa. Enzi ambazo wanasiasa walitumia makabila yao kutimiza malengo yao ya kisiasa zilitumbukiza nchi katika umwagikaji wa damu.
Kauli za wanasiasa za kufufua ukabila wakijifanya wanaupiga vita zinafaa kupigwa darubini Wakenya wanavyofanya kupitia mitandao ya kijamii hadi njama yao ishindwe.
Siasa za ukabila zinanufaisha watu wachache tu wanaotumia wengi wa jamii zao na kisha kuwasahau wakishawatumia kutimiza malengo yao. Mada ya ukabila inafaa kupigwa marufuku katika mikutano ya kisiasa.
Leave a Reply