WAANDAMANAJI walioshiriki maandamano dhidi ya mauaji ya wanawake #EndFemicideKe katika jiji kuu la Nairobi, walilazimika kukimbilia usalama wao baada ya polisi kuwarushia vitoa machozi.
Watu kadhaa wakiwemo wanahabari waliripotiwa kujeruhiwa na wengine kukamatwa katika maandamano hayo yaliyofanyika jana.Waandamanaji walikusanyika kuadhimisha Siku ya Haki za Binadamu Duniani na kukamilika kwa Siku 16 za Uanaharakati dhidi ya Dhuluma za Kijinsia (GBV).
Maandamano yalianzia Bustani ya Jeevanjee yakapita jijini hadi makao makuu ya idara ya mahakama ambapo kesi iliwasilishwa kuhusu kukithiri kwa mauaji ya wanawake nchini.
Waandamanaji walikusanyika saa tatu asubuhi lakini kufikia saa nne asubuhi, polisi walikuwa wamefika kutawanya umati wakitumia vitoa machozi.
Watu kadhaa walikamatwa akiwemo mkurugenzi wa shirika la Amnesty International, Irũngũ Houghton, na watetezi wengine wa haki za kibinadamu.
Washiriki walitawanyika na kukusanyika katika barabara ya Stewart Lane lakini wakarushiwa vitoa machozi tena katika makabiliano yaliyoendelea hadi adhuhuri na kusababisha biashara kwenye barabara ya Muindi Mbingu na Kenyatta Avenue kufungwa.
Taifa Leo haikuweza kubainisha ikiwa waandamanaji waliarifu polisi kabla ya kushiriki maandamano.
Chama cha Mawakili Nchini (LSK), Amnesty International, na wanaharakati wa haki za kibinadamu kupitia taarifa ya pamoja walikemea vikali kukamatwa kwa waandamanaji waliokuwa wamedumisha amani wakitaka polisi wawajibike.
“Walikamatwa kwa njia isiyo ya haki licha ya kushiriki maandamano kwa amani,” walisema watetezi wa haki.
“Inspekta Jenerali wa Polisi ni sharti aanzishe uchunguzi huru kuhusu ghasia na kukamatwa haramu na waliohusika wabebe msalaba wao.”
“Tunasimama pamoja na watu jasiri walioandamana leo licha ya ukatili uliowakabili. Vitendo vya polisi vinaashiria haja ya kuangazia kwa dharura mauaji ya wanawake, kuwalinda wanawake na kuhakikisha uwajibikaji kwa wanaotekeleza unyama huo.”
Hali ilikuwa tofauti Nyeri, huku waandamanaji wakisindikizwa na polisi hadi katika afisi ya Naibu Kamishna wa Polisi Kaunti hiyo.
Wanawake Kilifi waliitaka afisi ya Rais kutangaza dhuluma na mauaji ya wanawake kuwa janga la kitaifa.
Kisii, wanaharakati walikusanyika katika afisi ya Kamishna wa Kaunti kabla ya kuandamana mitaani wakiitaka serikali kuimarisha sheria zinazolinda maisha.
Nao wanaharakati Homa Bay walijumuika na maafisa kutoka idara ya mahakama, serikali ya kaunti na idara ya huduma za watoto na kuandamana kutoka Rangwe hadi Pap Kalango ambapo mkutano dhidi ya GBV ulifanyika.
Kadhalika katika Kaunti ya Siaya, wanaharakati walilaani visa vya GBV nchini na kuitaka serikali kuwalinda wajane.
Hii ni mara ya pili maandamano kama hayo yamefanyika mwaka huu.
Visa vya mauaji ya wanawake vilipokithiri Januari, makundi mbalimbali ya wanaharakati yaliandamana kwa lengo la kukomesha uovu huo.
Kinyume na maandamano ya awali yaliyofanyika kwa amani, shughuli hiyo jana iligubikwa na michafuko, makabiliano na polisi, uharibifu, majeraha na taharuki.
Ripoti za Daniel Ogetta, Moraa Obiria, Ndubi Moturi, Jackson Ngari, Mercy Mwende, Maureen Ongala, Wycliffe Nyaberi, George Odiwuor na Kassim Adinasi
IMETAFSIRIWA NA MARY WANGARI
Leave a Reply