Kiswahili ni mojowapo nyenzo za utambulisho wa Jamhuri ya Kenya – Taifa Leo


LEO ni Sikukuu ya Jamhuri. Siku ya Jamhuri ni mojawapo ya siku za kitaifa katika Jamhuri ya Kenya. Jamhuri ni nchi huru inayojitawala.

Kenya inatambuliwa kama Jamhuri na mataifa mengine ulimwenguni. Katiba ya Kenya ya 2010, inataja wazi kuwa Kenya ni Jamhuri inayojitawala.

Lugha ni mojawapo ya vipengele vinavyoitambulisha Jamhuri. Katiba ya Kenya ya 2010, inaeleza kwamba lugha ya kitaifa ya Jamhuri ya Kenya ni Kiswahili. Kwa hivyo, Kiswahili ni nyenzo inayoitambulisha Kenya kama Jamhuri. Kiswahili kama lugha ya taifa hutumiwa katika mikutano nchini kuwaunganisha wananchi kutoka maeneno mbalimbali nchini.

Tunaposherehekea Sikukuu ya Jamhuri, ni muhimu kutambua Kiswahili kama lugha ya kukuza utangamano nchini. Tukumbuke kuwa hotuba nyingi katika mikutano ya sherehe za Jamhuri Dei zitatolewa kwa Kiswahili. Hii ni kwa sababu Kiswahili ndiyo lugha ya kukuza utaifa, uzalendo na utangamano nchini.

Kiswahili ni lugha ya walio wengi. Kiswahili ni lugha ya wananchi katika Jamhuri ya Kenya. Kwa sababu ya umuhimu wa Kiswahili katika sherehe za Jamhuri Dei, mara nyingi hotuba ya Rais wa Jamhuri hutafsiriwa kwa Kiswahili. Watumishi wa serikali wanaomwakilisha Rais katika daraja mbalimbali za kiutawala wanatarajiwa kuwasomea wananchi hotuba ya Rais kwa lugha inayoeleweka na wengi. Lugha hiyo ni Kiswahili.

Mojawapo ya utambulisho wa Jamhuri ni lugha rasmi zinazotumiwa katika shughuli za kiserikali katika Jamhuri husika. Katiba ya Kenya ya 2010 inataja wazi kwamba lugha rasmi za Jamhuri ya Kenya ni Kiswahili na Kiingereza. Ni jambo la kujivunia kwamba Katiba ya Kenya inatambua Kiswahili kuwa lugha rasmi ya Jamhuri. Tunaposherehekea Sikukuu ya Jamhuri, juhudi za kimaksudi zinahitajika ili kukifanya Kiswahili kiwe lugha rasmi ya kweli kiutekelezaji katika Jamhuri ya Kenya.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*