MSANII wa Bongo, Diamond Platnumz, amevunja kimya chake kufuatia hatua yake ya kutotumbuiza katika tamasha la Furaha City Festival jijini Nairobi.
Msanii huyo inasemekana alipokea kitita cha dola 150,000 (takriban Sh19.3 milioni) ili kupamba hafla hiyo lakini akaondoka ukumbini bila kutumbuiza, na ameweka wazi kuwa hatarejesha donge hilo.
Katika video iliyoelekezwa kwa mashabiki wake, Diamond anaeleza kuwa yeye hufuata kikamilifu sera zake za utendakazi, ikiwa ni pamoja na kuheshimu muda uliopangwa.
“Siwezi kulipwa dola 150,000 kisha nije kupigana kutumbuiza jukwaani,” alisema.
“Nitafika ukumbini kwa wakati kusubiri mwandalizi wa hafla aniite jukwaani, nitaendelea kuangalia saa yangu, na muda wangu wa kutumbuiza ukiisha nitatoka nje ya ukumbi huo na sirudishi pesa zozote.”
Diamond alisisitiza kuwa hajihusishi na mabishano na wasanii wengine au waandalizi ili kupata nafasi yake jukwaani.
“Sihitaji kujadiliana na waandalizi au kupigana na wasanii wengine ili niruhusiwe kutumbuiza. Hiyo sio nidhamu yangu,” alisema kwenye video hiyo.
Mwimbaji huyo pia alizungumzia madai yaliyotolewa na msanii wa Kenya Willy Paul, ambaye anadai kuwa uongozi wa Diamond ulimzuia kutumbuiza ili kuruhusu nyota huyo wa Tanzania kupanda jukwaani kwanza.
“Itakuwa upumbavu kwangu kufanya hivyo; ina maana gani?” Diamond alihoji.
“Mimi ndiye mhusika mkuu, ambayo ina maana wasanii wengine wote wanaigiza kabla yangu. Willy Paul anajaribu tu kutengeneza drama kwa sababu bado anatafuta umaarufu. Huu ni upuuzi—muziki unahitaji bidii na usimamizi mzuri, si ushupavu na huruma.”
Alisema kuwa alifika mapema na kusubiri kwenye gari lake, kwani anapendelea kutokaa nyuma ya jukwaa.
“Tangu nilipofika kulitokea fujo ambazo hazikuisha, meneja wangu alimpigia simu mratibu kumuuliza kwa nini kuna fujo nyingi na kwanini mambo hayakusimamiwa ipasavyo, alijibu na kusema alihitaji dakika 10 zaidi. Kwa bahati mbaya, ghasia zilfika mahali nilipoketi,” Diamond anaelezea.
Hali ilipozidi kudorora, meneja wa Diamond aliamua ni bora amrudishe hotelini kwake.
“Kulikuwa na fujo pande zote za hafla, na sielewi kwa nini ilifanyika,” anasema.
“Msanii hawezi kutumbuiza chini ya hali kama hizi, na wengine wanaweza kuiona kama kukosa heshima.”
Diamond anasema alisubiri kwa takribani saa tatu bila kupanda jukwaani, akieleza kusikitishwa kwake lakini akathibitisha kuwa hakuwa na la kufanya.
Wakati huo huo waandalizi wa tamasha wamejitetea.
“Tunasikitika sana kutangaza kuwa Diamond Platnumz hakutumbuiza katika tamasha la Furaha City kama ilivyopangwa, sisi tukiwa waandalizi tulijitahidi yeye na timu yake walikuwa sawa, kuhakikisha mipango na dharura zote zilishughulikiwa ili kusiwe na matatizo.. Hata hivyo tabia na matakwa ya timu yake yalionekana kuwa ya kusikitisha na ya kupindukia kupita kiasi,” ilisema taarifa hiyo.
Huku wakikiri kulitokea suala dogo la kiusalama linalomhusisha msanii mwingine, walifafanua, “Tulitatua kwa haraka na kuhakikisha kwamba tamasha iliendelea kwa njia salama na ya kitaaluma. Tunaamini katika kuwatendea wasanii wote usawa na kudumisha viwango vya ubora wa juu kwa kila mtu anayehusika.”
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply