Serikali ilianzisha amri kali na sheria mpya ili kukomesha uuzaji na matumizi ya pombe haramu nchini, hatua ambayo ilisababisha kufungwa kwa maeneo kadhaa ya kuuza pombe.
Kampeni hiyo, iliyoongozwa na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, ilifuta leseni za wazalishaji na wasambazaji wa pombe ili wahakikiwe upya.Miezi tisa baada ya msako huo ambao uliwazuia maafisa wa umma kuendesha baa, biashara ya pombe haramu inaendelea kushamiri tena.
Kikosi cha mashirika mbalimbali kinachoongozwa na maafisa wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) kilinasa pombe haramu inayokisiwa kuwa na thamani ya zaidi ya Sh6.9 milioni mjini Maua, Kaunti ya Meru.
Kamishna wa Uchunguzi na Utekelezaji wa Sheria wa KRA, Bw David Yego, alisema vileo hivyo vilihifadhiwa katika nyumba ya kukodi eneo la Ikuru, Maua. Mnamo Jumatatu, katoni kadhaa za pombe kali na nembo bandia za ushuru zilinaswa Mang’u, mji wa Thika, Kaunti ya Kiambu.
Maafisa hao waligundua kiwanda haramu cha kutengeneza pombe, ndani ya nyumba ya kibinafsi eneo la Kiamumbi, Kaunti ya Kiambu.
“Katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, vifaa vya mamilioni vya kutengeneza pombe haramu na tani kadhaa za vinywaji vya pombe pamoja na ethanoli iliyosafirishwa kwa njia haramu vimenaswa katika msako unaoendelea,” alisema Bw Yego.
“Kuna viwanda vitatu vya pombe vilivyoanzishwa kinyume cha sheria, katoni 1,000 za pombe haramu, lita 56,000 za ethanoli, na nembo bandia 60,000 za ushuru zimenaswa katika maeneo mbalimbali nchini wakati wa oparesheni hiyo,” aliongeza Bw Yego.
Msako huo unahusisha mashirika mbalimbali ambayo yanajumuisha maafisa wa polisi, wanachama wa Chama cha Vileo Kenya (ABAK), na maafisa wa utawala ili kukabiliana na biashara ya pombe haramu inayoendelea.
Katika eneo la Mlima Kenya, ambapo tatizo la pombe haramu limekuwa shida kubwa, mambo yanaendelea kama kawaida huku siasa zikichukua nafasi kuu.
Katika eneo la Mathira, Kaunti ya Nyeri, sheria kali zilizowekwa kudhibiti uuzaji na unywaji wa pombe zimepuuzwa baada ya Mbunge wa eneo hilo, Bw Eric Wamumbi, kuwaagiza wamiliki wa baa kuendesha shughuli zao kama kawaida.
Bw Wamumbi alimlaumu Bw Gachagua kwa kuwalenga wamiliki wa baa wa eneo hilo kwa kuagiza kufungwa kwa biashara zao kinyume cha sheria.Bw Gachagua baadaye aliwalaumu maafisa fulani wa serikali kwa kuvuruga azma yake ya kukomesha ulevi katika Mlima Kenya.
Mnamo Juni mwaka huu, Bw Gachagua alitangaza kuwa vita dhidi ya pombe haramu zilikuwa zimeleta matokeo mazuri miongoni mwa vijana.
Leave a Reply