MNAMO Septemba 13, 2021, kampuni ya Burqa Ventures inasemekana kupokea kiasi kisichojulikana cha pesa kutoka Kaunti ya Marsabit kwa huduma zilizotolewa.
Ndani ya saa chache, kampuni hiyo iligundulika kuwa ilitoa Sh700,000 kutoka akaunti yake na kuzituma kwa kampuni nyingine ya Northern City Coaches Ltd.Northern City Coaches Ltd inamilikiwa na Alamitu Guyo Jattani – mmoja wa wake wa gavana wa Marsabit Mohamud Ali.
Kampuni hiyo inamiliki kundi la mabasi yanayotumia njia ya Nairobi-Marsabit-Moyale.Katika kisa kingine, kampuni ya Qoorti Ltd inadaiwa kutuma Sh300,000 kwa mke wa gavana huyo baada ya kulipwa na Kaunti ya Marsabit.
Qoorti Ltd inamilikiwa na Godana Halake, msaidizi wa kibinafsi wa gavana.Mtiririko huu wa pesa sawa na huo umeibuka miongoni mwa wanakandarasi kadhaa wa kaunti, na hivyo kusababisha Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuanza uchunguzi kuhusu kile wanachoamini kuwa huenda ni kashfa zinazodaiwa kulipwa gavana huyo na familia yake.
Bw Ali na zaidi ya wafanyakazi kumi wa kaunti wamerekodi taarifa na EACC, ambayo inachunguza makosa ya ununuzi katika kaunti ya Marsabit, kuanzia 2013.
Uchunguzi huo unaweza kuwafanya maafisa kadhaa wa zamani na wa sasa kushtakiwa, huku upelelezi wa awali ukionyesha kwamba walipa kodi wangeweza kupoteza angalau Sh8 bilioni kutokana na mitandao mingi ya ufisadi katika kaunti hiyo.
‘Uchunguzi ulianza 2023 na unaendelea. Tume haiwezi kutoa maelezo kwa wakati huu,” msemaji wa EACC Eric Ngumbi alisema.Mnamo Agosti, EACC iliomba Northern City Coaches Ltd kusalimisha kandarasi zozote au hati zingine zinazohalalisha pesa ambazo mwanakandarasi wa kaunti alituma pesa kwa kampuni hiyo inayomilikiwa na jamaa za gavana.Haijabainika ikiwa Northern City Coaches imewapa wachunguzi stakabadhi za kuthibitisha.
Taifa Jumapili hata hivyo, imefahamu kwamba mgongano wa kimaslahi na matumizi mabaya ya ofisi vinaongoza orodha ndefu ya mashtaka ambayo yanaweza kupendekezwa dhidi ya watu kadhaa.Nyingine ni pamoja na ukiukaji wa sheria za ununuzi na kupata mali ya umma kwa njia haramu.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply