Wakenya waponyoka na nafasi tano za kwanza Malaga Marathon huko Uhispania – Taifa Leo


VINCENT Kipkorir ndiye mshindi wa mbio za Generali Malaga Marathon nchini Uhispania mnamo Jumapili, Desemba 15, 2024.

Aliongoza Wakenya wenzake Micah Kipkosgei, Andrew Rotich, Genicious Rono na Josphat Menjo kuchukua nafasi tano za kwanza, mtawalia.

Kipkorir alinyakua taji kwa saa 2:08:05 nao Kipkosgei na Rotich wakakamilisha mbio hizo za kilomita 42 kwa saa 2:09:21 na 2:10:20 katika nafasi tatu za kwanza, mtawalia.

Nambari moja hadi tano walituzwa Sh406,710, Sh271,140, Sh135,570, Sh94,899 na Sh67,785, kwa usanjari huo.

Naye Daniel Simiu aliridhika na nafasi ya pili kwenye mbio za Tata Steel Kolkata World 25K nchini India baada ya kupoteza taji lake.

Mwanariadha wa Uganda awika

Mganda Stephen Kissa alinyakua taji kwa saa 1:12:33 na kufuatwa na Simiu (1:12:37), Anthony Kipchirchir (1:12:55), bingwa wa Tokyo Marathon Benson Kipruto (1:13:25), Asbel Rutto (1:13:36) na Hillary Mosop (1:13:56).

Muethiopia Sutume Kebede alitetea ubingwa wake katika kitengo cha wanawake kwa 1:19:17 baada ya kumaliza mbele ya Mkenya Viola Chepngeno (1:19:44), Mbahraini Desi Jisa (1:21:29).

Nchini Thailand, Winfridah Moseti alitawala 21km kwenye mashindano ya Bangsaen21 Half Marathon kwa 1:10:01 akifuatiwa na Rebecca Chelangat kutoka Uganda, bingwa wa Tokyo Marathon mwaka 2023 Rosemary Wanjiru (1:10:53), Gladys Chepkurui (1:11:11) na Antonina Kwambai (1:12:01), Jumamosi.

Wakenya wanne walimaliza ndani ya sita-bora katika kitengo cha wanaume. Bingwa wa London Marathon Alexander Mutiso aliridhika na nafasi ya pili kwa 1:02:34 nao Geoffrey Kipchumba (1:02:36), Justus Kangogo (1:03:55) na Erick Rotich (1:04:24) wakawa nambari tatu, tano na sita, mtawalia. Muethiopia Nibret Bogale alitwaa taji kwa 1:02:32.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*