BAADHI ya wasimamizi wa mashirika ya umma eneo la Nyanza sasa wanalaumu wanasiasa kwa kuzidisha changamoto katika Bima ya Afya ya Jamii (SHIF).
Viongozi hao wanakashifu baadhi ya wanasiasa wakiwatuhumu kwa kueneza habari potovu kuhusu SHIF.
Mwenyekiti wa Mamlaka ya Ustawi wa Maji eneo la Ziwa Victoria Kusini Odoyo Owidi, Mwanachama wa Bodi ya Mamlaka ya Kusambaza Dawa Nchini (KEMSA) Hesborn Omollo na Afisa Mkuu wa Chuo cha Utabibu nchini (KMTC) Dkt Kelly Oluoch, walisema siasa hazifai kuingizwa katika masuala ya SHA.
“Ni kawaida kwa mpito kutoka kwa mfumo mmoja hadi mwingine kukumbwa na vizuizi. Changamoto zote katika SHA zinashughulikiwa,” akasema Bw Owidi.
SHIF ilianzishwa ili kuchukua nafasi ya Bima ya Afya ya Kitaifa (NHIF) mnamo Oktoba 1
Tangu bima mpya ianze, kumekuwa na matatizo mengi hasa wakati hospitali zinadai malipo kutoka kwa SHA baada ya kuhudumia wagonjwa.
Huku serikali ikiambia wananchi mfumo huu ni bora zaidi, kuna viongozi ambao wanautaja kuwa mbovu na ghali.
Bw Owidi amewahimiza Wakenya wajisajili na kupuuza kauli za wanasiasa wanaokashifu SHA.
“Ina manufaa kadhaa ambazo hazikuwa katika NHIF kwa kuhusisha tiba ya magonjwa sugu ambayo awali hayakushughulikiwa,” akasema.
Viongozi hawa wa mashirika ya serikali waliandamana na wafanyakazi wenzao katika ibada ya maombi kanisani Oneno Nam Seventh Day Adventist eneo la Rachuonyo Kaskazini, Kaunti ya Homabay walipowarai wakazi wajisajili katika SHIF.
“Nia ya wanasiasa wanaopinga bima mpya na serikali ya Kenya Kwanza ni kumchafulia Rais William Ruto jina ili kujinufaisha kisiasa,” akasema Bw Owidi.
Mr Owidi aliendelea kuvumisha bima ya SHA dhidi ya NHIF akisema inawafaa wananchi wenye mapato ya chini.
“Ada ya chini ya SHA ni Sh300 ikilinganishwa na Sh500 ambazo zilitozwa Wakenya chini ya NHIF. Inawezekana sasa kwa familia zenye mapato ya chini kujiunga na bima mpya,” akaongeza.
Akikariri kauli za Bw Owidi, Bw Omollo alisisitiza kuwa Wakenya wote wana nafasi ya kunufaika na bima nafuu.
“NHIF ilikuwa inasaidia watu wachache lakini SHA itasaidia familia nyingi,” akasifu Bw Omollo.
Kulingana na Dkt Oluoch, NHIF ililazimisha baadhi ya watu kugharamia tiba walipokuwa wanalipa ada za hospitali.
“Hakuna haja ya kuwa na gharama zaidi chini ya SHA. Bima mpya itashughulikia gharama zote za tiba,” Mkuu wa KMTC alisema.
Hata hivyo, kumekuwa na malalamishi miongoni mwa Wakenya wanaopitia changamoto za kulipia matibabu licha ya kusajiliwa katika SHA.
Imetafsiriwa na Labaan Shabaan
Leave a Reply