Wakazi walivyomchinja mamba na kumtoa mtoto aliyemezwa Isiolo – Taifa Leo


WAKAZI wa kijiji cha Bulesa, eneo la Merti katika kaunti ya Isiolo wamemuua  mamba  aliyemshambulia na kummeza mvulana mmoja aliyekuwa akilisha mifugo wao karibu ni mto Ewaso Ng’iro.

Walipasua tumbo la mnyama huyo wa majini na kutoa mwili wa Hassan Jaldesa, 13, aliyefanya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Sita (KPSEA) mwaka huu.

Mwili huo ulizikwa Ijumaa kufungamana na desturi za dini ya Kiislamu.

Mvulana huyo alishambuliwa na mamba huyo Alhamisi siku ya Jamhuri Dei alipiga mbizi ndani ya mto Ewaso Ng’iro kutuliza makali ya jua.

Hapo ndipo aliposhambuliwa na mamba aliyekamata guu lake, akamburuta kisha akammeza.

Kisa hicho kiliwakasirisha wakazi waliojihami kwa silaha mbalimbali na kuanza kuwinda mamba huyo.

Bw Galgalo Malicha, mmoja wa jamaa wa mwendazake, alisema zaidi ya wakazi 100, wengi wao vijana walikongamana karibu na mto huo, wakashambulia mamba wa kwanza lakini iligeuka kuwa hakuwa muuaji.

“Baadaye watu hao ambao walikuwa na mapanga na mikuki walishambulia mamba mwingine ambaye alikuwa mhusika. Walipasua tumbo lake na kuondoa mwili wa Jaldesa,” akasema Bw Malicha.

Chifu wa Kata ya Bulesa Hassan Guyo alithibitisha kisa hicho alisema watu watatu walijerujuhiwa katika kukurukakara hizo na wamelazwa katika Hospitali ya Kaunti ya Isiolo ambako wanapokea matibabu.

“Mvulana mmoja, Ali Roba aligongwa na mkia wa mamba na kujeruhiwa mbavu. Anapokea matibabu hospitalini. Wengine wawili waliumwa mikononi na wanatibiwa katika kituo kimoja cha kiafya,” akaeleza Bw Guyo.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*