Wakongwe walia ngumbaru imesahaulika CBC ikipewa kipaumbele – Taifa Leo


WAZEE katika Kaunti ya Lamu wamelalamikia kusahaulika kwa elimu ya watu wazima, almaarufu ngumbaru.

Wazee hao wamedai kwamba katika miaka ya hivi majuzi, serikali na Wizara ya Elimu imeipa kipaumbele utekelezaji wa mtaala mpya wa CBC ilhali ngumbaru haikumbukwi.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu, Mohamed Mbwana, alishikilia kuwa elimu ya watu wazima ni kiungo muhimu kwenye mipango ya maendeleo ya taifa lolote lile. Alisema elimu hiyo ni muhimu kupewa uzito sawa na elimu nyinginezo zinazotiliwa mkazo.

Wanafunzi wakihudhuria darasa katika kituo cha mafunzo ya watu wazima cha Kapserton Adult Basic Education Centre eneo la Kipkaren Celian mjini Nandi mnamo 2013. PICHA | MAKTABA

Bw Mbwana alieleza kutoridhishwa kwake na jinsi wazee wengi Lamu bado hawajui kusoma na kuandika, hali ambayo inawaathiri kimaisha na hivyo pia kuathiri maendeleo ya kitaifa.

“Elimu ya ngumbaru ililetwa nchini kusudi likiwa ni kuleta nuru hasa kwa wengine wetu ambao tulidhania hatutajua kusoma au kuandika maishani. Mimi binafsi imenisadia pakubwa.

“Ila miaka ya sasa hatujaona tena msukumo wa elimu ya watu wazima. Utasikia kote mkazo ukiwekwa kwa mtaala wa CBC. Sisi wazee mumetuweka wapi? Lazima mtuzingatie pia. Ni muhimu elimu ya ngumbaru itiliwe mkazo pia,” akasema Bw Mbwana.

Wanafunzi wa Sekondari Tangulizi wakati wa somo ndani ya maabara ya sayansi katika Shule ya Msingi ya Bomu eneo la Changamwe mjini Mombasa, mnamo Januari 2024. PICHA | KEVIN ODIT

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Lamu, Bw Zachary Mutuiri, aliwataka wazee wajiandikishe kupokea elimu hiyo akisisitiza kuwa serikali inaithamini.

Alisema elimu ya ngumbaru inaendelea na akawataka wazee wenye kiu ya elimu hiyo kujitokeza.
“Wanaolalamika huenda hawajajitokeza wazi kujisajili kupokea mafunzo ya ngumbaru. Elimu ya ngumbaru ipo Lamu. Wazee hata wana afisa wao maalumu.

“Ningewasihi wenye kiu ya elimu hiyo wajitokeze na watahudumiwa,” akasema Bw Mutuiri.

Kassim Shee, 75, mzee wa Kizingitini, Lamu Mashariki, anataja kutojua kusoma na kuandika kuwa kikwazo kikubwa katika harakati za kuimarisha huduma za jamii nchini.  Anasema ari yake ni kutafuta hiyo elimu ya ngumbaru kwani miaka ya ujana wake hakuweza kukanyaga darasani.

Kinachomtia wasiwasi ni mahali pa kuipata elimu hiyo, akidai kuwa kwao Kizingitini hajaona kituo chochote au mwalimu wa ngumbaru wa kuwawezesha kuipata elimu wanayotafuta.

Watahiniwa wenye umri wa watu wazima na wa kibinafsi baada ya kumaliza mtihani wa mwisho wa KCPE 2015 katika Shule ya Msingi ya Nyamasaria mjini Kisumu. PICHA | MAKTABA

“Nina kiu ya elimu niliyoiacha miaka mingi iliyopita. Nataka kurudi darasani ila hawa walimu au vituo vya ngumbaru hatuvioni tena. Serikali ifanye juhudi kutuanzishia upya mpango huo. Wasitusahau,” akasema Bw Shee.

Kwa upande wake, Bi Khadija Hussein, 56, anasema hatua ya wanawe na wajukuu wake kuongea Kiingereza mfululizo kila wanapokaa naye kunamfanya kuwa na msukumo wa kutaka kurudi darasani, asome na kuifahamu vyema lugha hiyo.

“Sitaki kusengenywa mimi. Watoto na wajukuu zangu wanapoongea Kingereza nyumbani ninahisi upweke. Siwezi kuchangia kwa sababu sijui hata kinachozungumziwa. Na ndiyo sababu nataka nirudi ngumbaru, nisome ili nijue angalau neno moja moja la Kiingereza,” akasema Bi Hussein.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*