MGENI angetua Kenya Alhamisi na amsikize Rais William Ruto akiorodhesha mafanikio ya serikali yake tangu aingie mamlakani angedhani Kenya ni “ahera”.
Angedhani Kenya ni nchi ambapo kila kitu ki shwari na wananchi wote wanafurahishwa na kazi nzuri inayotekelezwa na serikali.
Kwenye hotuba yake alipoongoza taifa kwa sherehe za Jamhuri Dei katika Uhuru Gardens, Nairobi, alieleza namna serikali imetekeleza sera bora zilizoongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo na hivyo kupunguza gharama ya maisha.
Kulingana naye, kigezo cha kupungua kwa gharama ya maisha ni kushuka kwa kiwango cha mfumko wa bei kutoka asilimia 9.7 mnamo 2022 hadi asilimia 2.8 Oktoba mwaka huu.
Aidha, Dkt Ruto alitaja tangu aingie mamlakani serikali yake imewasaidia Wakenya 243,000 kupata ajira ng’ambo, wengine 200,000 wamepata ajira kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu huku maelfu ya vijana wakipata ajira kupitia majukwaa ya mitandao.
Isitoshe, Dkt Ruto alieleza namna serikali ilivyoweka rekodi ya kuajiri jumla ya walimu 56,000 ndani ya miaka miwili pekee.
Alipokuwa akielezea haya na mafanikio mengine katika mpango wa afya kwa wote kupitia bima mpya ya SHA, Dkt Ruto alitumia lugha nzito huku akiwakaripia vikali wakosoaji wa serikali ambao juzi aliwataja kama “wajinga”.
Lakini namshauri rais kwamba atulize hasira na ajaribu kuelewa uhalisia wa maisha ambayo Wakenya wengi wanaishi.
Achambue kwa makini taarifa anazopokea kila mara kutoka Shirika la Kitaifa la Ujasusi (NIS) haswa hisia za Wakenya kuhusu utawala wake.
Achambue ripoti zilizotolewa mwaka huu na asasi za serikali kama vile Benki Kuu ya Kenya (CBK), Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinazoonyesha kuwa kampuni nyingi zinafuta kazi wafanyakazi kutokana na kupanda kwa gharama ya kuendeshaji biashara.
Hali hiyo inachangiwa na kupanda kwa viwango vy ushuru, kupanda kwa gharama ya kawi na sera zingine kandamizi zinazotekelezwa na serikali hii.
Matokeo yake ni kwamba, kampuni nyingi zinazima shughuli zao nchini Kenya na kuhamia nchi jirani za Tanzania, Uganda na Rwanda.
Rais Ruto pia hasemi ukweli anapodai bei ya bidhaa za kimsingi kama vile unga wa mahindi zimeshuka ilhali ni wazi kuwa bei za bidhaa zimekuwa zikipanda kuanzia mwanzoni mwa Novemba.
Tasnifu yangu ni kwamba Kenya inapoadhimisha miaka 61 tangu ilipopata uhuru wa kujitawala, viongozi waliotangulia na hawa wa sasa wameshindwa kabisa kuikomboa taifa hili kiuchumi.
Leave a Reply