MWANASIASA Jimi Wanjigi amepuulizia mbali handisheki ya Rais William Ruto na mtangulizi wake Rais mstaafu Uhuru Kenyatta akisema meli ya serikali ya Kenya Kwanza inazama na haiwezi kuokolewa.
Katika mahojiano na Taifa Leo Jumatatu, Bw Wanjigi alidai ukuruba kati ya viongozi hao pamoja na Kiongozi wa ODM Raila Odinga unasukumwa na maslahi ya kibinafsi.
Kulingana na mwaniaji huyu wa urais 2022, uchumi wa nchi uko katika hali mbaya.
“Serikali imetuumiza kupitia ushuru mwingi pasipo uwajibikaji wala mwananchi kuona manufaa yoyote,” akasema Bw Wanjigi akihisi kuwa Dkt Ruto anatafuta msaada kutoka kwa Bw Kenyatta ili ajikomboe.
“Ruto anakaribisha watu wengi katika serikali yake ili wamsaidie meli isizame. Lakini hawezi kufaulu kwa sababu Uhuru hawakilishi sauti ya wananchi wa eneo la Mlima Kenya,” akaongeza.
Kuhusiana na kiongozi wa nchi kufanya kazi na viongozi wa upinzani, Bw Wanjigi alisema kuwa haitamfaa kitu akisema Wakenya wengi wamechoshwa na jinsi nchi inaendeshwa.
“Wakenya wanataka suluhu kwa matatizo ya kiuchumi. Hapa ndipo palipo uongozi wa kweli,” akaeleza.
Kadhalika, Bw Wanjigi alifunguka kuhusu uvamizi wa polisi katika makazi yake mnamo Agosti 2024. Alikumbana na hali hii katika utawala wa Rais Kenyatta na sasa pia utawala wa serikali ya Kenya Kwanza iliyoingia mamlakani 2022.
Bw Wanjigi alijisifu kuwa uvamizi huo haukuwa na mashiko ya kisheria aliposhukiwa kufadhili maandamano yaliyoendeshwa na vijana wa kizazi cha Gen Z Juni 2024.
Makazi yake ya Muthaiga yalivamiwa na polisi waliodai kuwa alimiliki silaha kinyume cha sheria.
“Hakuna jinsi serikali mbili zilizofuatana zingenivamia jinsi zilivyofanya na bado haziwezi kunipeleka mahakamani. Ni kwa sababu hazina ushahidi wowote kuhusu madai yao,” akajitetea.
Kinyang’anyiro cha AUC
Katika mahojiano hayo, Bw Wanjigi alimtakia heri Bw Odinga katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ifikapo Februari 2025.
Lakini mwanasiasa huyo anayemezea mate urais, anahisi kuwa iwapo Bw Odinga atashindwa katika uchaguzi huo, itakuwa pigo kubwa sana kwake.
“Anaweza kupagazwa kuwa mtu ambaye hushindwa kila wakati. Ila ninamjua Bw Odinga kwa miaka mingi na ana uwezo wa kujirejesha na kuwa imara tena,” akasema akieleza kuwa Kenya itakuwa na fahari iwapo ataibuka mshindi.
Hata hivyo, Bw Wanjigi hana imani kuwa uhusiano kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga utadumu baada ya uchaguzi wa AUC.
Kulingana naye, waziri mkuu wa zamani amemshikilia kiongozi wa nchi zaidi ya jinsi Bw Uhuru atampiga jeki.
“Ruto atakuwa na changamoto kubwa sana kwa vile ni Raila anamshikilia. Lakini kitu cha muhimu sasa ni kuokoa wananchi dhidi ya machungu wanayopitia,” akahitimisha.
Leave a Reply