SHUGHULI ya kuchimba dhahabu iligeuka kuwa msiba baada ya watu wanne kufariki katika mgodi mmoja ulioko eneo la Lami kwenye barabara kuu ya Lodwar-Kitale, Kaunti ya Pokot Magharibi, Jumanne asubuhi.
Waliofariki ni wanaume watatu na mwanamke mmoja. Mchimbaji mwingine alijeruhiwa vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kapenguria.
Kisa hicho kilitokea mgodi ulipoporomoka wakati watano hao walikuwa wakichimba madini hayo ya thamani kubwa.
Chifu wa eneo la Nasolot, Michael Mwotor, alisema wawili hao walikuwa wakichimba dhahabu kabla ya vifusi kuporomoka na kuwaua.
“Miguu ya aliyenusuriika kifo ilivunjika na alikimbizwa hospitalini,” alisema Bw Mwotor.
Chifu huyo alisikitika kwamba njaa imesukuma wakazi katika shughuli za kuchimba dhahabu licha ya kufahamu vyema kwamba walikuwa wakihatarisha maisha yao.
“Wanaume hao walikuwa wakitafuta dhahabu ili kupata pesa za kununua chakula lakini kwa bahati mbaya walikufa,” alieleza afisa huyo wa utawala.
“Wanatembelea mashimo ya dhahabu kila siku. Majirani walisikia kilio na kukimbia hapo kujaribu kuwaokoa. Kwa bahati mbaya wanne hao walikuwa tayari wamefariki,” akaongeza.
Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Pokot, Nelson Omwenga, akithibitisha mkasa huyo alisema miili ilitolewa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kapenguria.
Mbunge wa Sigor, Peter Lochakapong, aliomba uchunguzi ufanywe kuhusu tukio hilo huku akirai wakazi kusaka njia mbadala za kutafuta riziki.
Vifo hivyo vimejiri baada ya kamati ya uchimbaji madini kuundwa katika kaunti hiyo ili kusaidia kukabiliana na shughuli haramu ambazo zimekithiri mno eneo hilo.
Kamishna wa Kaunti ya Pokot Magharibi Khaliff Abdullahi alisema bado wanaandaa ripoti kamili kuhusu mkasa wa Jumanne.
“Tumekuwa tukiambia wakazi wasijihusishe na uchimbaji madini haramu lakini ni wazi ujumbe huo hausikiki. Ni lazima tukomeshe shughuli hii haramu,” akasema Bw Khaliff.
Leave a Reply