![TF-CAF-TUZO-2-1320x1584.jpg](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2024/12/TF-CAF-TUZO-2-1320x1584-678x381.jpg)
STRAIKA Ademola Lookman aliandikisha historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kutoka klabu ya Atalanta nchini Italia kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka inayotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), baada ya kubeba gongo la mwaka huu kwenye hafla iliyofanyika jijini Marrakech, Morocco.
Kama kawaida hakuna Mkenya, Mtanzania wala Mganda au mchezaji kutoka kanda ya Afrika ya Mashariki na Kati (Cecafa) alitinga orodha ya wawaniaji kwenye tuzo hizo za mwaka huu zilizoandaliwa Jumapili usiku.
Badala yake orodha hiyo ilijumuisha Lookman, Simon Adingra wa Ivory Coast (anasakatia Brighton ya Uingereza), Serhou Guirassy wa Guinea (anasakatia Borussia Dortmund ya Ujerumani), Achraf Hakimi wa Morocco (anasakatia PSG ya Ufaransa) na Ronwen Williams wa Afrika Kusini (anasakatia klabu ya nyumbani Mamelodi Sundowns).
Lookman alikuwa katika orodha ya wawaniaji wa tuzo ya Mwanasoka Bora Duniani maarufu Ballon d’Or 2024 na kumaliza katika nafasi ya 24.
![](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2024/12/TF-CAF-TUZO-1-scaled.jpg)
Anafuata nyayo za raia mwenzake wa Nigeria, Victor Osimhen, aliyeibuka bora barani Afrika mwaka 2023.
Mafanikio yaliyomfanya awapiku wawaniaji ni kuongoza Atalanta kushinda Ligi ya Uropa na pia kufikisha Super Eagles ya Nigeria katika fainali ya Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cote d’Ivoire. Osimhen na mshindi wa mwaka 2022 Mohamed Salah hawakuwa katika orodha ya wawaniaji.
Msimu huu wa 2024-2025, Ademola tayari amechana nyavu mara 11 (mabao manane kupitia mguu wa kulia, matatu mguu wa kushoto, mawili vichwa na penalti moja) katika michuano 19 katika mashindano yote. Amepeana asisti tano. Timu yake ya Atalanta inaongoza Ligi Kuu ya Italia baada ya mechi 16 za kwanza.
Ademola alisakata soka yake katika klabu ya Charlton, Everton, Fulham na Leicester nchini Uingereza na Leipzig nchini Ujerumani kabla kunyakuliwa na Atalanta mnamo Agosti 4, 2022. Alizaliwa mjini London, Uingereza na wazazi kutoka Nigeria.
![](https://informationcentre.co.ke/wp-content/uploads/2024/12/TF-CAF-TUZO-4-scaled.jpg)
Orodha ya washindi wa tuzo za CAF:
Mwanasoka Bora wa Mwaka (mwanamume) – Ademola Lookman (Nigeria & Atalanta)
Mwanasoka Bora wa Mwaka (mwanamke) – Barbra Banda (Zambia & Orlando Pride)
Chipukizi Bora wa Mwaka (mwanamume) – Lamine Camara (AS Monaco/Senegal)
Chipukizi Bora wa Mwaka (mwanamke) – Doha El Madani (ASFAR/Morocco)
Timu Bora ya Taifa ya Mwaka (wanaume) – Cote d’Ivoire
Timu Bora ya Taifa ya Mwaka (wanawake) – Nigeria
Klabu Bora ya Mwaka (Wanaume) – Al Ahly (Misri)
Klabu Bora ya Mwaka (Wanawake) – TP Mazembe (DR Congo)
Mwanasoka Bora wa Mwaka anayecheza Afrika (mwanamume) – Ronwen Williams (Mamelodi Sundowns/Afrika Kusini)
Mwanasoka Bora wa Mwaka anayecheza Afrika (mwanamke) – Sanaa Mssoudy (ASFAR/Morocco)
Kipa Bora wa Mwaka (mwanamume) – Ronwen Williams (Mamelodi Sundowns/Afrika Kusini)
Kipa Bora wa Mwaka (mwanamke) – Chiamaka Nnadozie (Paris FC/Nigeria)
Kocha Bora wa Mwaka (mwanamume) – Emerse Fae (Cote d’Ivoire)
Kocha Bora wa Mwaka (mwanamke) – Lamia Boumehdi (TP Mazembe)
Goli kali la mwaka 2024 – Cristovao Mabululu (Angola vs Namibia)
Leave a Reply