IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa Kenya imewatahadharisha Wakenya wanaoishi katika maeneo mbalimbali nchini kujiandaa na mvua kwa muda wa siku saba zijazo kuanzia Desemba 18 hadi Disemba 25.
Mkurugenzi Mkuu wa idara hiyo, Dkt David Gikungu, Jumatano Desemba 18, alitangaza kwamba Wakenya wanaoishi Nyanda za Juu Mashariki na Magharibi mwa Bonde la Ufa, Bonde la Ziwa Viktoria, Bonde la Ufa la Kati na Kusini, Kusini-mashariki na Pwani watashuhudia mvua.
Dkt Gikungu katika ushauri wake alisema kuwa kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka na Nairobi zitapata mvua za wastani hadi kubwa.
Katika maeneo hayo mvua itanyesha alasiri baada ya vipindi vya jua na mawingu asubuhi. Mvua za alasiri zilitarajiwa kunyesha hadi jioni.
Kaunti za Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet, Nandi, Nakuru zilitarajiwa kukumbwa na mvua kubwa kwa siku tano zijazo.
Idara hiyo ilitangaza kuwa kaunti zilizotajwa hapo juu zitapata mvua kubwa inayoambatana na ngurumo za radi huku wakazii katika maeneo hayo wakihimizwa kuwa macho kwa kuwa mafuriko yanaweza kutokea.
Kaunti zingine ambazo zinatarajiwa kukumbwa na hali sawa ya anga ni pamoja na Narok, Kericho, Bomet, Kakamega, Vihiga, Bungoma, Busia na Pokot Magharibi.
Zaidi ya hayo, mvua za wastani zinatarajiwa katika kaunti za pwani za Mombasa, Kilifi, Lamu na Kwale pamoja na maeneo ya pwani ya Kaunti ya Tana River.
Idara ya utabiri wa hali ya hewa katika ushauri wake wa kila wiki pia ilitahadharisha kuhusu hali ya baridi kali usiku katika kaunti za Nyandarua, Laikipia, Nyeri, Kirinyaga, Murang’a, Kiambu, Meru, Embu, Tharaka, na Nairobi.
Kulingana na idara ya hali ya hewa, halijoto usiku katika kaunti zilizotajwa hapo juu ilitarajiwa kushuka hadi 7°C katika siku tatu za kwanza za utabiri huo kabla ya kupanda hadi 11°C kwa siku zilizosalia.
Utabiri huo unaonyesha kuwa wakazi wanaoishi Siaya, Kisumu, Homabay, Migori, Kisii, Nyamira, Trans Nzoia, Baringo, Uasin Gishu, Elgeyo-Marakwet watavumilia
halijoto ya juu ya hadi 36°C mchana.
Kaunti zingine ambazo zilitahadharishwa kujiandaa kwa siku za joto ni pamoja na Marsabit, Mandera, Wajir, Garissa, Isiolo, Mombasa, Tana River, Kilifi, Lamu na Kwale.
Leave a Reply