WAZIRI wa Fedha John Mbadi kwa mara nyingine amesema hatamsaliti Rais William Ruto ambaye alimwamini na kumteua kuongoza wizara hiyo muhimu.
Bw Mbadi aliahidi Wakenya kwamba atafanya kila awezalo kuhakikisha hali ya uchumi wa nchi inaimarika na Rais Ruto atachaguliwa kwa muhula wa pili.
Bw Mbadi aliomba muda wa kutosha kufanya mabadiliko katika uchumi, akilaumu serikali iliyoongozwa na Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa baadhi ya matatizo ya kifedha ambayo yanakabili nchi.
Hata hivyo, alitaja muda wake mfupi katika wizara kama mojawapo ya bora zaidi katika historia akisema ameweza kufikia mengi ndani ya kipindi cha miezi minne ambacho amekuwa waziri.
Waziri huyo alisema hali ya uchumi si nzuri lakini ana imani mambo yataimarika.
Alisema mafanikio yake ofisini yatawezesha serikali ya Kenya Kwanza kuchaguliwa tena 2027.
Rais William Ruto anashinikizwa kupunguza gharama ya maisha.
Alimteua Bw Mbadi kutoka upinzani kuwa waziri wa fedha kama mojawapo ya mikakati yake ya kushughulikia matatizo yanayowakumba Wakenya.
Wakosoaji wake wanamshutumu kwa kukosa kutimiza ahadi alizowapa Wakenya wakati wa kampeni ambazo ni pamoja na kuunda nafasi za kazi na kurahisisha maisha kwa Wakenya.
Wakati wa sherehe za mwaka huu za Siku ya Jamhuri katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi, kiongozi wa nchi alitetea utawala wake akisema kuwa uchumi umekuwa bora zaidi katika miaka miwili iliyopita.
Bw Mbadi alimtetea Rais Ruto akisema hafai kulaumiwa kwa hali ya uchumi inayokumba nchi kwa wakati huu.
‘Kuna na changamoto katika nchi hii lakini sio mbaya kama ilivyokuwa wakati Uhuru Kenyatta aliondoka afisini,’ Waziri alisema.
Kulingana na Bw Mbadi, rais huyo mstaafu aliondoka madarakani wakati nakisi ya bajeti ya nchi kwenye Pato la Taifa (GDP) ilikuwa asilimia 8.1.
Waziri alisema utawala wa sasa umepunguza nakisi ya bajeti ya Pato la Taifa hadi asilimia 4.3.
‘Tunapozungumza, tumepunguza hadi asilimia 4.3. Mwaka ujao itakuwa asilimia 3.8 na tunapoelekea kwenye uchaguzi itakuwa chini ya asilimia tatu,” Bw Mbadi alisema.
Waziri huyo alisema amejaribu kuboresha uchumi wa nchi na hataiangusha serikali.
Alisema kuwa Rais Ruto alikuwa na imani naye na akaamua kumteua kuwa Waziri wa Fedha.
“Itakuwa vigumu sana kwangu kumsaliti. Sitalazimisha watu kuamini kwamba lazima Rais Ruto apate muhula mwingine kwa sababu hatuko kwenye mjadala huo sasa,” Bw Mbadi alisema.
Aliongeza “Nataka kumfanyia kazi na kurekebisha mambo. Tukisharekebisha makosa, tutakuja kwa Wakenya na kuwaomba nafasi nyingine ya kufanya kazi.”
Akizungumza wakati wa mkutano wa hadhara katika uwanja wa Chuo cha Mafunzo ya Udaktari cha Kenya katika Mji wa Ndhiwa, Bw Mbadi alisema amejaribu kuleta utulivu wa uchumi kupitia hatua zinazonuiwa kuhakikisha Wakenya hawakabiliwi na gharama ya juu ya maisha.
Inajumuisha kulipa mishahara ya wafanyikazi wa serikali kwa wakati na utoaji wa pesa za maendeleo na matumizi ya kawaida kwa kaunti.
Bw Mbadi alisema wafanyikazi wa serikali watalipwa ifikapo tarehe 18 kila mwezi.
Tunapozungumza leo, kaunti zote zimepokea mgao wa pesa. Nimewapa pesa hadi Novemba na hakuna malimbikizi huku mgao wa mwisho wa Sh 32.9 bilioni ukitolewa Jumatatu,” akasema.
Imetafsiriwa na BENSON MATHEKA
Leave a Reply