MASHINDANO ya mashua huwa kivutio cha watalii katika maziwa Baringo na Bogoria lakini mabadiliko ya hali ya hewa yameleta athari mbaya katika Kaunti ya Baringo.
Katika uzinduzi wa mashindano ya mashua ya Kaldich ziwani baringo, Gavana wa Kaunti ya Baringo Benjamin Cheboi alihimiza kuwepo kwa juhudi za pamoja kuvumisha sekta ya utalii inayopigwa na dhoruba
Kaunti hii ambayo inajivunia wanyama, maziwa, milima na visiwa ambavyo aghalabu huvutia watalii wa Kenya na ng’ambo, inalenga kutumia mbinu za mauzo kidijitali kuvutia watalii.
“Nilikutana na vijana wanaofanya kazi katika ufuo wa ziwa na kusikiliza wanachotaka kiimarishwe ili wanufaike. Tutaongeza juhudi katika kuvumisha vivutio vya utalii kutumia mitandao ya kidijitali,” akasema Bw Cheboi.
Mshindi wa mbio za boti ambayo yaliingia katika makala ya kumi mwaka huu, Bw Luis Juma, alisema mabadiliko ya hali ya hewa yameathiri vibaya vianzo vya uchumi Baringo.
“Mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha eneo hili imezamisha hoteli mbili za kifahari ambazo husaidia watalii wanaojivinjari,” akateta akisisitiza kuwepo kwa mikahawa mingine ambayo bado inaweza kuwafaa.
Kadhalika, wavuvi wamekuwa wakilalama kuwa samaki asilia wamepunguka katika Ziwa Baringo baada ya kumalizwa na aina nyingine za samaki kutoka mataifa ya Bara Asia kama vile China.
Kwa sababu ya upungufu huu, Bunge la Kaunti ya Baringo linashinikizwa kupitisha sheria ya kuhakikisha samaki wa kutosha wanaongezwa ziwani humo ili kuimarisha uchumi wa majini na utalii.
Leave a Reply