Duale akanyagia breki mwekezaji ndani msitu wa Karura – Taifa Leo


SERIKALI imeondoa leseni ambayo ilitolewa kwa Karura Golf Range ili ijenge maeneo ya kitalii na kujivinjari ndani ya Msitu wa Ngong.

Waziri wa Mazingira Aden Duale Jumatatu, Desemba 18, 2024 alisema kuondolewa kwa leseni hiyo iliyotolewa na Shirika la Misitu Nchini (KFS), ilitokana na kutolewa kwake bila sheria kuzingatiwa.

Kampuni hiyo ya gofu ilikuwa ijenge uwanja, hoteli na bustani ndogo ndani ya msitu huo.

“Nimeamrisha Afisa Mkuu wa Kitengo cha Utunzaji Misitu (CCF) na Mkurugenzi wa Mamlaka inayosimamia Mazingira Nchini (NEMA) iondoe leseni hizo mbili na kuanda maelezo ya kina ndani ya saa 72,” akasema Bw Duale kupitia mtandao wa X.

“KFS imeamrishwa ijizuie kutoa leseni zaidi na ukaguzi wa leseni zote ambazo zimewahi kutolewa utafanyika kwa ajili ya uwazi na uwajibikaji.”

NEMA ilikuwa imetoa leseni kwa kampuni hiyo mnamo Novemba 28, 2024 baada ya kufanya uchunguzi na utathmini wake wa kina. Leseni hiyo iliruhusu KFS na Kaunti ya Nairobi kupisha Karura Golf Range itumie ardhi ya msitu.

Pia, ilitoa masharti kuwa Karura Gold Range lazima izingatie masharti yote ya misitu huku ikisisitiza hakuna mti ambao unastahili kukatwa wakati wa utekelezaji wa mradi huo.

“Kama wizara tutatoa mwelekeo kuhusu suala hilo ambalo limevutia ghadhabu za umma. Hii itafanyika baada ya Mkurugenzi wa NEMA na afisa wa misitu kuniarifu kwa kina kuhusu mchakato wote unaozingira utata huu,” akaongeza Bw Duale.

Kauli ya Bw Duale imekuja baada ya Vuguvugu la kulinda misitu la Green Belt (GBM) kushtaki serikali kuhusiana na mpango wa kuondoa ekari 51.6 za ardhi ambayo ni sehemu ya msitu wa Karura.

Ardhi hiyo ilitolewa ili kusaidia katika upanuzi wa barabara ya Kiambu kwa thamani ya Sh38 bilioni. Vuguvugu hilo lilidai kampuni ya China ya Sinohydro imeingia kwenye mkataba na Mamlaka ya Kitaifa ya Ujenzi wa Barabara Kuu (KeNHA) kujenga barabara hiyo.

GBM ilisema kuwa upanuzi wa barabara hiyo bila kupata leseni ya athari zake kimazingira, ni kukiuka haki za raia kuwa na mazingira safi na mazuri.

Imetafsiriwa na CECIL ODONGO

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*