Wagonjwa taabani wauguzi wakigoma Hospitali ya Rufaa ya Kiambu – Taifa Leo


HUDUMA za afya zimesitishwa katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Kiambu baada ya wauguzi kuanza mgomo ulioathiri shughuli katika hospitali hiyo.

Wagonjwa waliachwa hoi wakitwikwa jukumu la kutafuta njia mbadala za kupata matibabu.

Katibu wa chama cha wauguzi tawi la Kiambu Dkt Hillary Kibiriti alidai zaidi ya wauguzi 300 hawajapokea mshahara kwa miezi miwili sasa.

Wanalalamika wakidai kuwa waliondolewa kutoka kwa mfumo wa malipo.

“Kufikia sasa tunasema imetosha kwa sababu punda amechoka. Wauguzi wakiondolewa kutoka kwa mishahara, haihusu tu malipo tu. Taasisi za fedha (kama vile benki) zinawasakama kulipa mikopo na pia wanakosa kupata huduma za bima ya afya,” akasema Dkt Hillary Kibiriti.

Wauguzi hawa waliandamana hadi katika afisi za Bunge la Kaunti ya Kiambu kuwasilisha malalamishi yao.

“Tumepokea stakabadhi zenye masuala ambayo mnataka yaangaziwe. Kwa hivyo mtasubiri kisha tuangalie tutakachofanya,” alisema afisa aliyepokea malalamishi.

Kupitia viongozi wao, wauguzi waliapa kutokomesha mgomo hadi malilio yao yasikilizwe na kutatuliwa.

Wahudumu hawa wa afya wanadai kupokea vitisho kutoka kwa maafisa wa serikali ya kaunti sababu ya kushiriki mgomo huo ambao umelemaza huduma za afya katika hospitali hiyo ya umma.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*