Uhuru hana uwezo wowote wa kumsaidia Ruto kisiasa – Taifa Leo


USIMWAMINI yeyote anayekwambia eti Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ndiye kigogo wa siasa za Mlima Kenya. Anayetoa dai hilo ama anakudanganya makusudi, au kabisa hajui siasa za eneo hilo zinavyopangwa.

Kalia jamvi nikupe ukweli wa mambo.

Wanaolazimisha dhana kwamba Bw Kenyatta ndiye kigogo huko wanajaribu kuwapa matumaini wafuasi wa Rais William Ruto, ambaye ametokea kuchukiwa mlimani kama nyama ya nguruwe Saudia.

Wanatamani sana Bw Kenyatta amrejeshee Dkt Ruto Mlima wote.

Hali ilivyo sasa hivi katika eneo hilo ni kwamba chuki ambayo kwayo Dkt Ruto anachukiwa na wakazi inaipiku ile ya kihistoria ambayo kwayo Bw Raila Odinga wa ODM amechukiwa huko tangu alipokosana na marehemu Rais Mwai kibaki mapema mwaka 2003.

Na kwa kuwa si siri tena kwamba ukuruba kati ya Dkt Ruto na eneo hilo uliisha alipotumia Bunge kumtimua aliyekuwa naibu wake, Bw Rigathi Gachagua, nitakwambia hivi: Machoni pa wakazi wa Mlima Kenya, Uhuru Kenyatta ameungana na adui yao mkuu, Dkt Ruto.

Kwa hilo Bw Kenyatta hatasamehewa kamwe. Kwa wakazi hao, hiyo ni ithibati tosha kwamba hawakukosea kabisa walipopinga jaribio lake la kuwashawishi wamchague Bw Odinga mnamo mwaka 2022.

Kwao ina maana kwamba Bw Kenyatta hana nia njema ya kulikomboa eneo hilo kisiasa; anajali maslahi yake pekee, hasa ikikumbukwa kuwa miezi kadha iliyopita aliteta vikali kwa kucheleweshewa malipo yake ya kustaafu.

Huhitaji kutumia akili nyingi kujua kwamba Bw Kenyatta, ambaye alishindwa kumsaidia Bw Raila Odinga kuupata urais mnamo mwaka 2022, hana uwezo wowote wa kulishawishi eneo la Mlima Kenya kurejeleana na Dkt Ruto.

Utengano huo ni wa kati ya sasa na milele. Mlimani hakutoki msamaha wa kisiasa, hasa ikiwa aliyewakosea si mmoja wao. Anachukuliwa kuwa msaliti daima.

Ndivyo huko kulivyo, wala usiniulize kwa nini.

Nimeandika na kurudia kwenye ukurasa huu kwamba tofauti na maeneo mengineyo kote nchini, mkondo wa siasa za Mlima Kenya hutegemea mapenzi ya wakazi wa kiwango cha chini kabisa. Wao, na wala si viongozi wao, ndio wanaoamua watamuunga nani mkono.

Huenda Bw Gachagua, ambaye kwa sasa anatamba kisiasa huko hata baada ya kung’olewa madarakani, hataruhusiwa kuwania wadhifa wowote wa umma kwa mwongo mmoja ujao, lakini eneo hilo halina upungufu wa viongozi.

Linaweza kumteua mmoja leo na kumpa ugogo kesho.

Vile-vile, linaweza kumkweza Bw Gachagua hadi kiwango cha kigogo mkuu, limpe jukumu la kulitafutia washirika wa kisiasa ili kumkabili Dkt Ruto na washirika wake.

Kumbuka hili ni eneo ambalo halijali kamwe limo ndani au nje ya serikali. Maslahi yao yakiwa hatarini – hata ikiwa mmoja wao ndiye anayeyahatarisha – watampinga na kumkimbia mchana jua la utosi.

Lilimtia adabu Bw Kenyatta alipoungana na Bw Odinga, seuze Dkt Ruto.

Usione ajabu kwamba mtandaoni kumeanza kutokea vibonzo vya kudhihaki na kutukana muungano mpya kati ya Dkt Ruto, Bw Kenyatta na Bw Odinga, tena vikawa maarufu ghafla!

Kimoja kati ya vingi ambavyo nimeviona kinawasawiri watatu hao wakiwa ndani ya dau, nahodha akiwa Dkt Ruto, kisha dau lenyewe linapewa jina la ‘Mv Mapepo’!

Hao ni watu ambao hawaogopi chochote. Wamekinai diplomasia.

Tayari, Bw Gachagua amepuuzilia mbali ushirika huo mpya na kuliweka eneo la Mlima Kenya hasa, na Kenya nzima kwa jumla, katika hali ya taharuki kwa kuahidi kutoa tangazo muhimu la kisiasa ifikapo mwezi Januari, 2025.

Kana kwamba kutuzidishia taharuki, Bw Gachagua anasema: “Tunawahimiza watu waendelee kukutana. Hatuwezi kuwazuia. Tutakapotoa tangazo letu hapo Januari, kila mtu atajua kuwa hata nasi tumekuwa tukikutana.”

Kati ya sasa na mapema mwaka ujao, nchi nzima itasalia katika hali hiyo ya taharuki kwa kuwa ni wakati huo pia ambapo Bw Odinga anatarajiwa kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) katika uchaguzi utakaofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Ushindi au ushinde wa Bw Odinga unatarajiwa kuwa na athari kuu kwa siasa nchini Kenya. Wakenya wengi ambao hawapendi jinsi Dkt Ruto anavyoongoza nchi wanatia dua Bw Odinga ashindwe ili arejee nchini, akosane na Dkt Ruto, na aanze kuisumbua serikali yake.

Bw Odinga akishindwa kisha akosane na Dkt Ruto kwa sababu yoyote ile, kuna uwezekano mkubwa kwamba Bw Odinga atajiunga na muungano wa kisasa atakamokuwa Bw Gachagua. Huenda humo pia atakuwamo Bw Kalonzo Musyoka wa chama cha Wiper.

Hatimaye, huenda Dkt Ruto akabaki na Bw Kenyatta pekee, na kila mtu anajua hakuna msaada mkubwa wa kisiasa ambao Bw Kenyatta anaweza kumpa.

Kenya ni nchi ya siasa kali, wakati mwingine mseto wa maudhi na burudani, ila muhimu zaidi ni kwetu sisi wananchi wa kawaida kuhakikisha kuwa hatutumiwi na wanasiasa kuivunja nchi yetu.

[email protected]



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*