AFC Leopards washawishi Wanyama awasakatie kabla ya kustaafu – Taifa Leo


JUHUDI za kumshawishi kiungo Victor Mugubi Wanyama achezee timu ya AFC Leopards zinaendelea kuchacha baada ya nahodha huyo wa klabu ya CF Montreal nchini Canada kudai kwamba angependa kusakatia timu ya nyumbani kabla ya kustaafu.

Wanyama ambaye alichezea Leopards kati ya 2006 na 2007 kabla ya mwaka uliofuata kujiunga na Helsingborg IF ya Sweden ameagana na CF Montreal baada ya mkataba kutamatika.

Kiungo huyo mahiri mwenye umri wa miaka 33 alijiunga na CF Montreal mnamo 2020 akitokea Tottenham Hotspur ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kutokana na ujuzi wake wa miaka mingi kwenye soka ya kulipwa, staa huyo alitarajiwa kuurefusha mkataba wake ili aendelee kuchezea CF Montreal, lakini akakataa huku akisisitiza kwamba angependa kumalizika shughuli hiyo nyumbani.

Lakini hadi sasa, haijajulikana ni timu gani anayolenga nyota huyo, wala hajasema iwapo tayari amefanya mazungmzo na timu yoyote kabla ya dirisha la wachezaji kuhama kufunguliwa rasmi mwezi ujao wa Januari, 2025.

Mara tu baada ya kupata habari hizo, mwenyekiti wa klabu ya AFC Leopards, Dan Shikanda amejitokeza kudai kwamba klabu yake inamshawishi kiungo huyo avae jezi la Leopards kwa mara nyingine.

“Tunataka arejee nyumbani achezee timu ‘ya mama’ iliyomfanya akafahamika kote duniani.”

Kabla ya kujiunga na Leopards, Wanyama alichezea Nairobi City Stars ya mtaa wa Kawangware kwa muda mfupi.

“Tunamuomba kwa unyenyekevu arudi nyumbani kutuchezea kabla ya kustaafu,” alisema Shikanda huku akiongeza kwamba uwepo wake kikosi utapandisha motisha wa wachezaji watakaotaka kucheza soka ya majuu kama yeye.

Shikanda alisema Leopards iko tayari kabisa kumkaribisha nyota huyo anayesemekana kuwa miongoni mwa wanasoka tajiri nchini na hata Afrika Mashariki na Kati.

“Tunamtaka aje ainue jina la klabu kwa dunia nzima inayomfahamu,” alisema Shikanda.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*