WATU wanaoishi mijini wanafika kijijini kwa sherehe za Desemba kwa bashasha, wakitumia pesa nyingi walizochukua mikopo, kununua vitu vingi ambavyo hawahitaji, na kuburudisha marafiki kwa lengo la kujinata tu.
Wengine huwa wanawasili wakiendesha magari ya kukodi; hakuna ubaya wowote na hilo, lakini wanajifanya kana kwamba wanamiliki Jeep au Toyota V8. Yote kuteka hisia katika kijiji.
Tabia hiyo inakumbatiwa zaidi na tabaka la kati, na mara tu sherehe zinapomalizika, wanavunjika moyo na kuwa na wakati mgumu kulipa bili.Kulingana na mkurugenzi wa kampuni ya Rwathia jijini Nairobi, Kanene Kabiru, msimu wa sherehe huja na ubadhirifu ambao huwaacha watu wengi na uchungu wa kutumia fedha kiholela lakini faida kwa wachuuzi na wafanyabiashara
“Ninapokuambia kuwa msimu wa sherehe huja na wazimu wa matumizi, nichukulie kwa uzito,” Bw Kabiru ambaye hufanya biashara ya kuuza pombe, chakula na nyumba za kulala wageni, aliambia Taifa Leo
“Kwa kawaida, huwa tunaongeza maradufu lengo letu la mauzo wakati wa msimu wa sikukuu ili wafanyakazi wetu wachukue tahadhari na kuwashawishi wateja zaidi,” asema.
Baada ya matumizi kama hayo, Bw Kabiru anafichua kuwa kuna wale ambao baadaye huingia katika afisi ya meneja ili kufanya mazungumzo ya kurejeshewa pesa
“Mvulana hutumia zaidi ya Sh200,000 kutoka usiku wa kuamkia Krismasi hadi Mwaka Mpya, kisha anajitokeza baadaye, akiwa na kitabu cha kumbukumbu akiomba kurejeshewa takriban Sh10,000 ili kutatua shida yake ya kifedha,”asema.
Alipata funzo
Bw Michael Nduati, mhasibu, ni mmoja wa watu ambao walipata funzo baada ya kutumia pesa kiholela msimu wa sherehe.
“Ilikuwa 2021. Nilifika nyumbani kwangu Ngurwe-ini nikiwa na Sh100,000. Nilikuwa na umri wa miaka 30 wakati huo, nilikuwa barobaro bila familia,” anasema.
Bw Nduati alikuwa amekodi gari, ambalo lilimgharimu Sh2,000 kwa siku. “Ningetumia Sh2,000 za ziada kwa siku kununua mafuta.
Kwa siku nane, nilipoteza pesa na kukwama kijijini kwa miezi miwili” aliambia Taifa Leo.
Alikuwa akianza siku yake kwenye baa ya mtaani akiburudisha kundi la marafiki wa kijijini wenye kiu ya pombe. Kisha angehamia mji wa karibu wa Kabati kwa ushujaa zaidi.
Siku ya sita ya sherehe, aliishia kusababisha ajali, akakamatwa, akashtakiwa kwa kusababisha kifo kwa kuendesha gari kiholela, na akazuliwa rumande kwa miezi miwili.
“Wakati nilipomalizana na mahakama, nilikuwa nimefutwa kazi yangu Nairobi, na kampuni ya kukodisha magari ilikuwa ikidai zaidi ya Sh300,000 kama ada ya ukarabati kwa kuwa kampuni ya bima ilikataa kufidia uharibifu,’”asema.
Mwaka mmoja baadaye, alipata kazi mpya.’Ninaogopa yanayokuja na likizo ya Desemba. Afadhali niende msituni kufunga na kuomba kuliko karamu,” asema.
Afisa mkuu wa polisi wa Kaunti Ndogo ya Kigumo Bw Kiprono Tanui anasema msimu wa sherehe huwafanya watu wengi kuwa wabadhirifu.
“Kila afisa wa polisi aliye na uzoefu atakuambia kuwa sherehe huja na matukio ya ajabu ya kifedha. Matukio ya kawaida yanayoripotiwa ni wavulana kumwagiwa pombe na hatimaye kupoteza pesa na vitu vya thamani,’”anasema.
Kupeana pesa
Anaongeza kuwa baadhi ya watu wanaotoka mjini huibiwa kwa vile wana tabia ya kupeana pesa nyingi kwenye baa. Wengine wanaonyesha pesa nyingi lakini wanakataa kulipa bili na kuishia kuandamana hadi vituo vya polisi na wamiliki wa baa.Kisha wengine hukopa pesa ili kutumia kwa sherehe.
Mary Karinga ambaye hukopesha pesa anasema Desemba ndio mwezi anaopata faida zaidi.Amekuwa katika biashara hiyo kwa miaka 12 na anasema huwa hakosi kupata angalau faida ya Sh100,000 kila Desemba.
“Biashara hii ya kukopesha fedha haina kinga ya kisheria. Kwa hivyo. inamaanisha lazima utafute dhamana nzuri kutoka kwa wateja wako. Wakati wa msimu wa sikukuu, wateja wangu wakuu ni wale kutoka mijini,” anasema. “Baada ya likizo ya Desemba, maduka yangu huwa yamejaa vitu kama vile laptop, simu za mkononi, vito na hata nguo za bei ghali,” anasema.
Bw Wanjumbi Mwangi, mtaalamu wa masuala ya fedha katika shirika la NewTimes anasema ukosefu wa nidhamu ya matumizi ndio chanzo cha mambo haya yote ya kipuuzi.
“Unapojikuta unaweka pesa ulizochuma kwa bidii kwenye mifuko yako na kuanza kuzurura mitaani kutafuta watu wa kuzitumia, huo unajulikana kama wazimu wa kiuchumi,”anasema.
Leave a Reply