IEK yamuonya Sudi dhidi ya kujiita mhandisi bila kusomea taaluma hiyo – Taifa Leo


NI hatia kutumia taji la “Mhandisi” bila kusomea taalamu ya uhandisi, wahandisi sasa wamemwonya Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi.

Kulingana na Rais wa chama cha Wahandisi Nchini (IEK) Mhandisi Shammah Kiteme, Sudi yu hatarini kupigwa faini ya Sh500,000 au asukumwe jela kwa miaka mwili, kwa kosa hilo.

Hii ni kwa mujibu wa Sheria ya Wahandishi Nchini ya 2011.

“Tafadhali zingatia kuwa taji la ‘Mhandisi’ kabla ya jina la mtu yeyote linalindwa na sheria; Sheria ya Wahandisi ya 2011. Inamchukua mtu miaka minane ya bidii kuipata. Oscar Sudi, tafadhali koma kutumia taji hili ambalo hujalipata kwa kusomea taaluma hii,” akaonya Kiteme kwenye ujumbe kupitia akaunti yake ya mtandao wa X.

Mnamo Jumamosi Desemba 21, 2024, Bw Sudi alitunukiwa Shahada ya Heshima katika Uongozi na Utawala na Usimamizi, kutoka Chuo Kikuu cha Kikristo cha NorthWestern.

Alipewa shahada hiyo katika sherehe ya kufuzu iliyofanyika katika uwanja wa  Chuo Anuai cha Kitaifa cha Eldoret, mjini Eldoret.

Lakini kwenye chetu chake, Sudi alirejelewa kama “Eng Oscar Kipchumba Sudi”, “Eng” ikiwa ufupisho wa jina la Kizungu “Engineer” yaani “Mhandisi”.

Kando na Bw Sudi, mbunge wa Sirisia alitunukiwa Shahada ya Heshima katika Usimamizi wa Umma na Sayansi ya Siasa huku Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alipewa Shahada ya Heshima katika Uongozi, Utawala na Usimamizi.

Uhalali wa masomo ya Bw Sudi umewahi kutiliwa shaka pale aliposhtakiwa kwa kughusi vyetu vya masomo.

Hata hivyo, kesi dhidi yake ilitupiliwa mbali Juni mwaka huu kwa ukosefu wa ushahidi wa kutosha.

Kimsingi, Shahada za Heshima, ambazo hazimhitaji mtu kusomea, hutolewa na vyuo vikuu kwa watu kutokana na michango yao katika vyuo hivyo, jamii na taifa.

Vyuo vikuu vya umma nchini na vile vya kibinafsi vimewahi kuwatunu watu mashuhuri shahada za heshima kwa michango yao katika jamii na taifa kwa ujumla.

Kwa mfano, mnamo mwaka wa 2004, Chuo Kikuu cha Nairobi kilimpa marehemu Profesa Wangari Maathai Shahada ya Heshima ya Uzamili katika Sayansi kutambua mchango wake katika utunzaji wa mazingira na huduma kwa taifa.

Ni mwaka huo ambapo Profesa Maathai alishinda Tuzo ya Nobel kwa mchango wake katika nyanja hiyo kuweka historia kama Mkenya wa kwanza kushinda tuzo hiyo inayoenziwa ulimwenguni.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*