MBUNGE wa Embakasi Mashariki Babu Owino amesema kuwa haogopi kufukuzwa ODM baada ya kufunguka na kusema amekuwa akitishiwa kutokana na kukataa kuunga serikali jumuishi.
Bw Owino alisema amemwaambia Kinara wa ODM Raila Odinga kuwa hawezi kuunga mkono serikali ambayo anahisi kuwa haithamini maslahi ya raia.
Mbunge huyo amesema kuwa haogopi kutimuliwa chamani na ataendelea kushikilia msimamo wake. Amesema ni mwenyezi Mungu ndio hutoa viongozi na waliomchagua walifanya hivyo kupitia mwongozo wa mwenyezi Mungu.
Awali akiwa mtetezi sugu wa Raila, Bw Owino ameonekana amekengeuka kisiasa tangu maandamano ya Gen Z mnamo Julai mwaka huu. Alikashifu vikali hatua ya ODM kushirikiana na utawala wa Rais William Ruto.
Mbunge huyo amesema kuwa yeye si mwoga wala haogopi kufurushwa chama hicho cha Chungwa. Bw Owino analenga ugavana wa Kaunti ya Nairobi na inakisiwa ukuruba kati ya Gavana Johnson Sakaja na Bw Odinga pia umemkoroga nyongo na kumfanya asijihusishe na chama tena.
“Nilikuwa namfanyia Raila kampeni lakini nilimwaambia siwezi kuunga serikali dhalimu kwa Wakenya. Niliambiwa kuwa nimemea pembe nitafukuzwa chamani,” akasema akiwahutubia wakazi wa eneobunge lake kwenye video ambayo imesambaa sana mitandaoni.
“Siogopi kufurushwa ODM. Hata wakinifukuza kutoka kwa chama kuna tatizo? Sasa niishi kwa hofu kwa sababu nitafukuzwa 2027?” akauliza kwenye mkutano na wakazi wa Mihangó Kayole.
Leave a Reply