HATUA ya Rais William Ruto kuwateua baadhi ya wandani wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa nyadhifa kuu katika serikali imewapa magavana saba matumaini kudumisha viti vyao katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Hii ni kwa sababu wanawachukulia baadhi yao, haswa magavana wa zamani, kama wapinzani wao wakuu katika kinyang’anyiro hicho.
Ndiposa, kwa mfano, magavana wanahudumu muhula wa kwanza kama vile Kimani Wamatangi (Kiambu) na mwenzake wa Nakuru Susan Kihika wameunga mkono uteuzi wa William Kabogo na Lee Kinyanjui kama mawaziri.
Bw Kabogo, aliyetunukiwa Wizara ya ICT na Uchumi wa Kidijitali alikuwa miongoni mwa wapinzani wakuu wa Bw Wamatangi katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Kiambu 2022.
Naye Bw Kinyanjui, alimkosesha usingizi Bi Kihika katika uchaguzi wa ugavana wa Nakuru mwaka huo.
Kimsingi, wapiga kura wa kaunti za Nairobi, Kiambu, Nakuru, Meru, Taita Taveta, Nyandarua na Isiolo hawajawahi kuwarejesha afisini magavana wao tangu kuanzishwa kwa utawala wa ugatuzi 2013.
Kaunti za Nairobi na Kiambu, zimeongozwa na magavana wanne kila moja, watatu katika kila moja ya mihula miwili iliyopita.
Bi Kihika alifurahia uteuzi wa Bw Kinyanjui kwa sababu anachukuliwa kuwa mpinzani wake mkuu, ikiwa angesalia katika upinzani, ikizingatiwa kuwa ushawishi wa serikali ya Kenya Kwanza unaendelea kupungua katika kaunti ya Nakuru inayochukuliwa kuwa sehemu ya Mlima Kenya.
Tangu kutimuliwa kwa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Bi Kihika amekumbana na hasira za wapiga kura waliomzomea katika hafla moja ya mazishi eneo bunge la Bahati, alipokuwa akisoma risala za rambirambi kutoka kwa Rais Ruto.
Katika kaunti ya Kiambu, uteuzi wa Kabogo umetoa afueni kidogo kwa Gavana Wamatangi ikizingatiwa kuwa pamoja na aliyekuwa Waziri wa Biashara Moses Kuria walikuwa wapinzani wake wakuu.
Kaunti ya Kiambu sasa ni ngome wa upinzani dhidi ya utawala wa Rais Ruto, uasi ukiongozwa na wandani wa Gachagua Seneta Karungo Thangwa na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wa Muchomba.
Wandani wengine wa Bw Gachagua wanatoka kaunti ya Nyandarua na wao ni; Seneta John Methu na Mbunge wa Kipipiri Wanjiku Muhia.
Gavana wa kaunti hiyo Moses Kiarie Badilisha pia anapambana kuondoa mkosi wa watangulizi wake kutofaulu kutetea viti vyao.
Katika kaunti ya Nairobi Gavana Johnson Sakaja hakuelewana na Bw Gachagua alipokuwa afisini.
Na baada ya kutimuliwa kwake Oktoba mwaka huu, Mbunge huyo wa zamani wa Mathira ameapa kuhakikisha kuwa Bw Sakaja anashindwa katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Bw Gachagua amemlaumu Gavana Sakaja kwa kubuni sera zinazoumiza wakazi wa Mlima Kenya, wanaoendesha biashara mbalimbali katika kaunti ya Nairobi.
Kabla ya kutimuliwa kwake, naibu huyo wa rais wa zamani aliongoza mkutano wa hadharia katika Soko la Muthurwa ambapo alipinga mpango wa kuhamishwa kwa wafanyabiashara wa mboga na matunda hadi soko jipya liliko kando la barabara ya Kangundo, eneo bunge la Embakasi Mashariki.
Leave a Reply