WATOTO waliokuwa wakiishi kwenye makao yao ya Kibra Pride, Nairobi wamejawa na furaha msimu huu wa Krismasi baada ya makao hayo kufunguliwa tena tangu yachomeke Septemba mwaka huu, 2024.
Shirika lisilo la kiserikali la Christian Best Camps limeshirikiana na jamii, wahisani na mashirika mengine kufungua tena makao hayo.
Yaliteketezwa na watu wasiojulikana, tukio ambalo nusra lisambaratishe maisha ya watoto hao kwa kuwa baadhi yao walipata majeraha mabaya.
Mnamo Jumapili, Desemba 22, yalifunguliwa tena huku watoto hao wakishukuru na kufurahia hatua hiyo baada ya kuhangaika, ikizingatiwa wengi wao ni mayatima.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Christian Best Camp, Erick Simba alisema kuwa makao hayo yamejengwa upya kisha yakapakwa rangi, yakawekwa kamera za CCTV na kompyuta, pamoja na walinzi na vilevile kuwekewa samani mpya.
“Baadhi ya watoto walichomeka na lilikuwa tukio baya, lakini tumewasaidia warejelee maisha yao kama zamani na hii ni tuzo bora zaidi kwao wakati huu wa Krismasi,” akasema Simba ambaye pia ni mwanachama wa bodi ya makao hayo ya watoto.
Chifu wa eneo hilo Nehemiah Mwocha alisema tukio la kuteketezwa kwa makao hayo lilisikitisha na sasa watamakinika kulinda watoto wasidhuriwe tena.
“Haya ni makao ya watoto yatima na tulikuwa na wasiwasi kuhusu hatima yao baada ya nyumba wanayoishi kuteketezwa. Tulihangaika na kuvunjika moyo kuhusiana na tukio hili, lakini sasa tumefurahi kutokana na msaada ambao tumepokea,” akasema Chifu Mwocha.
“Wale marafiki ambao wameshirikiana kuwapa watoto hawa makao wamefanya vyema sana. Tunaomba msaada zaidi ili kuwapa watoto hao maisha mazuri,” akaongeza Bw Mwocha.
Baadhi ya watoto walisimulia jinsi ambavyo walikuwa wameishi makao hayo na wakafurahi kwa kurejelea maisha yao ya awali.
Irene Khasandi ambaye ni mwanzilishi wa Kibera Pride Children’s Home alisema kuwa tangu 2013 wamekuwa wakiwasomesha na kuwatimizia mahitaji mengi, ikikumbukwa kuwa wengi wao hawana wa kutegemea.
“Tunashukuru waliotusaidia kurejesha makao haya, wabarikiwe na wale ambao wanataka kutusaidia wajitokeze zaidi ili tuwasaidie,” akasema Bi Khasandi.
Leave a Reply