VIONGOZI wakuu nchini wanatarajiwa kusherehekea Krismasi leo, Jumatano, maeneo mbalimbali huku ujumbe wa umoja na maridhiano ukitarajiwa kutawala hotuba zao makanisani siku hii muhimu.
Rais William Ruto, Kinara wa ODM Raila Odinga, Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ni kati ya viongozi wakuu ambao wataadhimisha siku hii muhimu maeneo tofauti.
Rais William Ruto amekuwa katika ngome yake ya kisiasa ya Uasin Gishu ambapo amekuwa akikita kambi kwenye Ikulu ndogo ya Eldoret.
Mnamo Jumatatu, Rais aliweka picha kwenye kurasa zake za mitandaon akiwapa watoto mayatima na wakazi zawadi ya Krismasi.
“Huu ni msimu mwingine wa kuwakumbuka wasiokuwa nacho na maskini katika jamii,” akaandika Rais Ruto kwenye ukurasa wake rasmi wa Facebook.
“Niliwapa Krismasi watoto kutoka makao mbalimbali Uasin Gishu na maeneo jirani kwenye Ikulu ndogo ya Eldoret,” akaongeza Rais.
Usiku wa kuamkia leo, Desemba 25, 2024 Rais alitarajiwa kuhutubia taifa ambapo angetoa ujumbe wake wa heri njema Wakenya wanaposherehekea Krismasi.
Hapo jana, Jumanne, Rais Ruto alikuwa katika shamba lake Kilgoris, Kaunti ya Narok ambako alikutana na Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) Moussa Faki.
“Nimekutana na Faki ambapo tumejadiliana kuhusu masuala mengi, ikiwemo uchaguzi unaokuja wa AUC ambao unawaniwa na Raila Odinga,” akasema Rais Ruto.
Kinyume na mtangulizi wake Rais Uhuru Kenyatta ambaye alikuwa akiadhimisha Sikuu ya Krismasi Mombasa, Rais Ruto amekuwa akisherehekea siku hiyo nyumbani kwake Sugoi, Uasin Gishu.
Bw Odinga naye yupo nyumbani kwake Opoda, eneobunge la Bondo Kaunti ya Siaya kama ada kwake kila msimu wa Krismasi.
Bw Odinga ambaye atatinga umri wa miaka 80 Januari 7, 2025 amekuwa nyumbani kwake tangu Jumatatu.
Kama tu Rais Ruto, pia anatarajiwa kutoa taarifa ya kuwatakia Wakenya sikukuu ya kufana.
Raila anatarajiwa kufungua mwaka Siaya ambapo atakuwa mwenyeji wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais William Ruto mnamo Januari 2, 2025 wakati wa kilele cha Tamasha ya Jamii ya Waluo na pia ufunguzi wa uga wa Jaramogi Oginga Odinga.
Bw Musyoka naye atakuwa Nairobi na familia yake baada ya kuadhimisha miaka 73 jana.
Bw Gachagua ambaye amekuwa na mwaka mgumu baada ya kung’atuliwa kwenye wadhifa wake, naye yuko nyumbani kwake eneobunge la Mathira, Kaunti ya Nyeri kwa Krismasi.
Leave a Reply