Viongozi wa kidini wataka serikali iwalipe kwa kutoa mafunzo – Taifa Leo


VIONGOZI wa dini za Kikristo na Kiislamu wanataka serikali izindue mpango wa kuwapa hela kidogo kutokana na majukumu wanayoyatekeleza katika jamii.

Wakihutubu katika Msikiti wa Masjid Majimaul katika mtaa wa Langas, Jijini Eldoret, walisema wanaendeleza mafunzo ya kidini kwa lengo la kudumisha maadili mema miongoni mwa wanafunzi nchini.

Barak Hamid Barak na Sheikh Mohamed Ali mmoja wa viongozi wa SUPKEM Mombasa, walisema iwapo walimu wa dini zote watalipwa kiasi fulani cha pesa wataboresha mafunzo yao na hivyo kuimarisha mafunzo yao ya kimaadili kwa kurejelea dini zote.

Walisema kuwa hatua hiyo itachangia pakubwa kuboresha maadili miongoni mwa chipukizi na hivyo basi kuwepo kwa kizazi ambacho kinaheshimu maadili siku za usoni.

Bw Barak alitaka serikali kujumuisha walimu wa shule za Jumapili, Sabato na Madrasa katika mpango huo ili kuona kuwa watoto kutoka katika dini zote wana maadili mema.

“Naiomba serikali ya Rais William Ruto ambaye ni mcha Mungu kuinua hali ya walimu wa dini kwa kushawisihi wabunge kuanzisha hazina ya kuwapa angalau kitu walimu hawa kama motisha ya kufundisha watoto wetu maadili,” alisema Bw Barak.

Maoni yao yaliungwa mkono na mwenyeji wao Sheikh Abubakar Bini, mwenyekiti CIPK Ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

“Ombi hili linapaswa kuhusisha walimu wote wa kidini iwe ni Wakrsito, Waislamu miongoni mwa dini zingine angalau walipwe Sh15, 000 kwa kutoa mafunzo hayo yanayojenga maadili miongoni mwa vijana,” akasema Sheikh Bini.

 

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*