KINYUME na inavyokuwa, kitovu cha jiji la Nairobi kimeendelea kuwa mahame msimu huu wa Krismasi 2024.
Maarufu kama CBD, Jiji la Nairobi siku za kawaida hushuhudia idadi kubwa ya watu.
Hata hivyo, Wakenya wakishabikia shamrashamra za Sikukuu ya kuzaliwa kwa Yesu Kristu, idadi ya watu wanaoonekana Jijini ni ya chini mno.
Hilo ni bayana kufuatia taswira ya barabara mbalimbali Jijini Nairobi.
Kwa mfano, Tom Mboya, barabara yenye shughuli tele za usafiri; matatu na magari ya kibinafsi yanayoingia na kutoka, hamna msongamano.
Kawaida, barabara hiyo hushuhudia msongamano kuanzia asubuhi hadi jioni.
Kituo cha matatu cha Koja, magari mengi ya huduma za umna yanayoegeshwa, Alhamisi, Desemba 26, 2024 ni machache tu yaliyoonekana.
Kimathi Street na Kenyatta Avenue, ni barabara zingine za Jiji ambazo aghalabu huwa na shughuli nyingi za usafiri na uchukuzi.
Ni magari machache yanaoonekana yakipita katika Kaunti hiyo inayoongozwa na Gavana Johnson Sakaja.
Maduka ya biashara nayo, taswira yake si tofauti na hali ya barabara ilivyo.
Ni wafanyabiashara wanaohesabika waliofungua.
Thika Super Highway, huwa yenye shughuli tele msongamano wa magari asubuhi ukiwa ratiba ya kila siku ila kwa sasa wanaoishi viungani mwa jiji inawachukua dakika chache kutua Nairobi CBD.
Kwa mujibu wa data za Shirika la Kitaifa kuhusu Takwimu (KNBS) za mwaka wa 2019, Kaunti ya Nairobi ina zaidi ya watu 4,397,073, idadi ikiwa imeongezeka kufikia sasa.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, wakazi wengi wa miji walisafiri mashambani msongamano ukishuhudiwa katika barabara kuu ya Nairobi na Nakuru.
Asubuhi ya kuamkia Desemba 25, Thika Road ilishuhudia msongamano sawa na Nairobi – Nakuru, kufuatia wakazi wa Nairobi wanaoishi Murang’a, Kirinyaga, Embu, Nyeri na Meru waliosafiri kuungana na jamaa zao mashambani.
Nauli nayo ilipanda mara dufu.
Leave a Reply