Wanahabari watano wauawa kwenye shambulizi la Israel huko Gaza – Taifa Leo


MAAFISA wa Gaza walisema shambulizi la anga la Israel liliwaua waandishi wa habari watano wa Kipalestina nje ya hospitali  Alhamisi, ingawa jeshi la Israel lilisema lilishambulia gari lililokuwa limewabeba wanamgambo Kiislamu.

Madaktari wamesema watu hao watano walikuwa miongoni mwa takriban watu 21 waliouawa katika mashambulizi ya anga ya Israel katika eneo hilo kabla ya alfajiri, huku Hamas na Israel zikirushiana lawama kutokana na kuchelewa kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano ya zaidi ya miezi 14.

Muungano wa Wanahabari wa Palestina umesema shambulizi moja liliwaua waandishi watano wa  Al-Quds Today waliokuwa kwenye gari la matangazo mbele ya Hospitali ya Al-Awda katika kambi ya wakimbizi ya Al-Nuseirat katikati mwa Gaza.

Video kutoka eneo la tukio ilionyesha mabaki  ya gari nyeupe na kile kinachoonekana kuwa mabaki ya neno “PRESS” katika rangi nyekundu kwenye milango ya nyuma.

Muungano huo umesema zaidi ya waandishi wa habari 190 wa Kipalestina wameuawa na  Israel tangu vita hivyo vilipoanza Oktoba 2023.

Shirika hilo lenye  makao yake makuu mjini Gaza limetaja shambulio hilo kuwa mauaji ya kinyama na kusema katika taarifa yake kwenye Telegram kwamba watano hao “waliuawa walipokuwa wakitekeleza wajibu wao wa kukusanya habari na kibinadamu”.

Jeshi la Israel lilisema “lilifanya shambulizi kwa usahihi kwenye gari lililokuwa na genge la kigaidi la Islamic Jihad ndani ya eneo la Nuseirat.”

Israel imekanusha mara kwa mara kuwalenga waandishi wa habari na kusema kuwa inachukua hatua za kuzuia kuwapiga raia.

Madaktari katika eneo hilo walisema watu wengine wanane waliuawa na wengine 20 kujeruhiwa katika shambulio la anga lililofanywa na Israel kwenye nyumba moja katika kitongoji cha Zeitoun, Gaza City. Idadi ya vifo inaweza kuongezeka kwani watu wengi wamenaswa chini ya vifusi, waliongeza.

Katika mji wa Gaza, shambulio la Israel kwenye nyumba moja katika kitongoji cha Sabra liliwauwa watu wanane zaidi, madaktari walisema, na kufanya idadi ya waliofariki Alhamisi kufikia 21.

Siku ya Jumatano, kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas na Israel walirushiana  lawama kwa kushindwa kwao kuhitimisha makubaliano ya kusitisha mapigano licha ya maendeleo yaliyoripotiwa na pande zote mbili katika siku zilizopita.

IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*