MAZISHI ya mwanablogu wa Meru Daniel Muthiani almaarufu Sniper, aliyefariki mwaka mmoja uliopita, yameahirishwa kwa muda usiojulikana kufuatia mzozo wa ardhi.
Marehemu Sniper, ambaye alitekwa nyara Desemba 2, 2023 na mwili wake kupatikana Mto Mutonga Tharaka Nithi, alipaswa kuzikwa leo Alhamisi, Desemba 27, 2024.
Hii ni mara ya pili kwa familia hiyo kuahirisha mazishi yake mwezi huu, baada ya ibada ya mwisho iliyokuwa imepangwa kufanyika Desemba 13 kuahirishwa kwa sababu ya kucheleweshwa kwa kupatikana kwa haki katika mahakama.
Mwili wa marehemu umelazwa katika chumba cha kuhifadhia maiti tangu Desemba 2023, baada ya familia na majirani kuapa kutouzika mwili huo hadi haki ipatikane.
Akizungumza na wanahabari siku ya Krismasi, Desemba 25, Bi Ann Kanjira, mama wa marehemu, alisema wamepokea vitisho kutoka kwa mfanyabiashara maarufu kuhusu ardhi ya familia hiyo.
“Nimepokea vitisho kutoka kwa mfanyabiashara anayedai kumiliki ardhi ya familia yetu. Anataka kuweka uzio kwenye shamba hili,” Bi Kanjira alisema.
Bw John Mutia, mwanafamilia alisema hati miliki ya ardhi ya familia ya marehemu iko mikononi mwa tajiri huyo wa eneo hilo.
“Tulipokuwa tukipanga mazishi ya marehemu mnamo Desemba 27, wazazi walipokea vitisho kutoka kwa Moses Lichoro. Ameiomba familia hiyo kuondoka katika ardhi yao. Tunataka kukabiliana na tishio kwa familia kabla ya kumlaza Muthiani,” Bw Mutia alisema.
Alisema familia hiyo iliripoti vitisho hivyo kwa polisi na wanasubiri hatua zichukuliwe.
Hata hivyo, Bw Lichoro alikanusha kutishia familia ya Sniper akisema alipata shamba hilo kihalali kutoka kwa babake marehemu.
“Kwa mara ya kwanza nilinunua ekari nne za ardhi kutoka kwa babake Sniper mwaka wa 2010 na tukapata hati miliki 2014. Ukweli ni kwamba babake marehemu alikuwa na ardhi ambapo aliishi na familia yake na ana hati miliki,” Bw Lichoro alisema.
“Mwaka jana, nilinunua sehemu ya ardhi kutoka kwa baba na hii ndiyo ardhi wanayozungumzia. Familia ilishuhudia shughuli hiyo. Nilimtuma meneja wa eneo kwa familia hiyo kuwaomba watengeneze uzio uliobomolewa. Sikutoa vitisho vyovyote kama ilivyodaiwa.”
Bw Lichoro alihusisha mzozo huo na tukio la Februari ambapo alipoteza mali ya thamani ya zaidi ya Sh50 milioni baada ya kundi la watu kushambulia biashara, nyumba na shamba lake huko Kabuitu.
Washukiwa kadhaa walifikishwa mahakamani kwa tuhuma za kuteketeza mali yake na kuharibu mashamba yake ya miraa.
Leave a Reply