KNCHR yasuta polisi kuhusu utekaji nyara – Taifa Leo


TUME ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) imekanusha ripoti ya Inspekta Jenerali wa polisi Douglas Kanja kwamba hakuna Wakenya waliotekwa nyara nchini ikisema katika mwezi wa Desemba pekee 2024, watu saba hasa watumiaji wa mitandao ya kijamii wametekwa nyara na kufikia sasa, sita hawajulikani waliko.

Mwenyekiti wa KNCHR Rosylene Odede alisema tume inaendelea kufuatilia mtindo unaotia wasiwasi wa utekaji nyara katika maeneo kadhaa ya Kenya. “Tume imebainisha kuwa utekaji nyara huu unaendelezwa kwa siri na watu wasiojulikana wakiwa na silaha. Tume inabainisha zaidi kwamba waliotekwa nyara wamekuwa wakosoaji ( serikali), hasa kwenye mitandao ya kijamii,” Bi Odede alisema kwenye taarifa. Alisema kumekuwepo na matukio kumi na tatu zaidi ya utekaji nyara au kutoweka kwa watu katika kipindi cha miezi mitatu na kufanya jumla ya visa vya utekaji nyara kuwa 82 kuanzia Juni 2024.

“Saba kati ya visa vya utekaji nyara vya hivi karibuni viripotiwa katika mwezi wa Desemba 2024 huku sita kati yao wakiwa bado hawajulikani waliko, hivyo kufikisha idadi ya watu ishirini na tisa (29) ambao hawajapatikana tangu Juni 2024,” alisema.

Aliongeza: “Tume, inalaani vikali utekaji nyara huu ambao uko nje ya Katiba. Utekaji nyara ni mateso, ukatili, udhalilishaji na unyanyasaji wa binadamu. Hauna nafasi katika nchi ya kidemokrasia kama yetu! Tume inatahadharisha kwamba ikiwa mtindo huu wa utekaji nyara utaendelea, basi tutakuwa tunarejea kwa kasi katika siku za giza za historia yetu ambapo matukio kama hayo yalikuwa yanaleta hofu kwa mtu yeyote anayeikosoa Serikali.”

Kulingana KNCHR, waliotekwa nyara Desemba 2024 ni Steve Kavingo Mbisi mnamo Desemba 17 kaunti ya Machakos, Billy Wanyiri Mwangi aliyetekwa 21/12/2024 kaunti ya Embu, Peter Muteti aliyetekwa akiwa Uthiru, Nairobi mambo Desemba 21 na Bernard Kavuli ambaye aliyetekwa akiwa Ngong Desemba 22.

Naomi almaarufu @Jabertotoo aliyetekwa Desemba huko Ruaraka, Nairobi alipatikana lakini Gideon Kibet almaarufu Kibet Bull aliyetekwa Desemba 25 na kaka yake Rony Kiplangat ambaye pia aliyekuwa nyara siku hiyo hawajapatikana.

“KNCHR inasisitiza uhuru na usalama wa mtu chini ya Ibara ya 29 ya Katiba inayohakikisha haki ya kutonyimwa uhuru kiholela au bila sababu za msingi, inayoharamisha kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashtaka, kuteswa na kutendewa ukatili, unyama au udhalilishaji,” alisema.

Alikumbusha Huduma ya Kitaifa ya polisi kwamba ni jukumu lake kulinda raia wote nchini.

“Tume ina wasiwasi kuhusu taarifa iliyotolewa na Inspekta Jenerali wa Polisi Desemba 26, 2024, ikisema kwamba polisi hawahusiki na utekaji nyara huo. Tunakumbusha Huduma ya Kitaifa ya Polisi kuhusu jukumu lake la kumlinda kila mtu nchini Kenya kutokana na vitendo hivyo vya kikatili hasa tukibainisha kuwa utekaji nyara huu unafanyika mchana kweupe, huku baadhi yao wakinaswa kwenye CCTV lakini bado hakuna mtu anayekamatwa,” alisema Bi Odede.

“Kwa hivyo Tume inapenda kukumbusha Serikali ya Kenya kwamba ina jukumu la kutekeleza kulinda haki na ustawi wa kila mtu nchini Kenya na haja ya kuweka kipaumbele kukuza na kulinda haki za kila mtu,” Tume iliongeza.

Tuma ilimtaka Inspekta Jenerali wa Polisi kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa kuharakisha uchunguzi ili Wakenya wajue ni nani anayeendeleza utekaji nyara huu na kuwalinda dhidi ya matukio kama hayo na kukamatwa wale wanaohusika. Vile vile , ilitaka wote waliotekwa nyara waachiliwe huru mara moja na bila masharti au kuwasilishwa mahakamani wakiwemo 29 ambao bado hawajulikani walipo.

Kwa mujibu wa mamlaka yake, Tume imekuwa na itaendelea na uchunguzi huru na kusaidia manusura na familia za waliotekwa nyara. Tume pia inatoa wito kwa umma kuripoti matukio yoyote ya ukiukaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na utekaji nyara kwa kutuma arafa kwa -22359,barua pepe- [email protected]; na Simu ya Bila malipo 0800720 627.

 

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*