Huzuni diwani mwingine wa Lamu akifariki baada ya kuugua – Taifa Leo


KAUNTI ya Lamu imejipata tena katika maombolezo baada ya Diwani Maalumu Rebecca Wambui Wainaina kuaga dunia.

Spika wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Azhar Ali Mbarak alithibitisha kifo hicho, akisema Bi Wainaina alifariki Alhamisi usiku wakati akipokea matibabu kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali iliyo Mombasa.

Bi Wainaina, 35, aliteuliwa kuhudumu kama diwani maalum katika bunge la Lamu kupitia chama cha Safina baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti, 2022.

“Niko na majonzi kutangaza kifo cha ghafla cha diwani maalum kwenye bunge la Lamu, Bi Rebecca Wambui Wainaina. Aliaga dunia Alhamisi usiku akipokea matibabu kwenye hospitaliya Pandya mjini Mombasa. Mola ailaze roho yake mahali pema peponi,” akasema Bw Mbarak.

Naibu Spika wa Bunge la Lamu, ambaye pia ni Diwani wa Wadi ya Mkunumbi aliyechaguliwa kupiti chama cha Safina, Bw Paul Kimani Njuguna, alimtaja marehemu kuwa mwenye bidii na mchapa kazi.

“Alikuwa kiongozi aliyejitolea pakubwa kuhakikisha haki za wananchi zinaheshimiwa vilivyo. Ni kiongozi aliyejitahidi kuinua hali ya chama chetu. Ni masikitiko kwamba tumempoteza. Mola awafariji wanafamilia wakati huu mgumu. Mungu ailaze roho ya Bi Wainaina mahali pema peponi,” akasema Bw Kimani.

Afisa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano na Uhusiano Mwema Katika Bunge la Kaunti ya Lamu, Bw Hussein Miji, alimuomboleza Bi Wainaina kama mtetezi aliyejitolea kuhakikisha haki za walemavu, akina mama na wasiojiweza katika jamii zinazingatiwa.

Pia anatambulika kwa kuwasilisha hoja bungeni zinazofungamana na hali ya usalama Lamu ikizingatiwa kuwa utovu wa usalama umekuwa donda sugu la muda mrefu kwa eneo hilo.

“Ni kiongozi mtetezi. Kila akisimama bungeni alitetea maslahi ya watu wanaoishi na ulemavu na jinsia ya kike. Isitoshe, suala la utovu wa usalama Lamu alikuwa akiliwasilisha kupitia hoja mbalimbali bungeni, azma yake ikiwa ni kutaka lishughulikiwe ili usalama na amani idumu Lamu. Tumempoteza kiongozi na mtetezi shupavu,” akasema Bw Miji.

Diwani maalum wa zamani wa Bunge la Kaunti ya Lamu, Bi Jane Ndung’u, alimuomboleza Bi Wainaina kuwa kiongozi aliyewajibikia majukumu yote, ikiwemo yale ya kifamilia, kisiasa na uongozi.

Bi Wainaina ni diwani wa pili katika Bunge la Kaunti ya Lamu kufariki mwaka huu.

Mnamo Mei, 2024, diwani mwingine maalum, Bi Zahara Shee wa chama cha ODM alifariki na kuzikwa katika kijiji chao cha Matondoni, Lamu Magharibi.

Kifo cha Bi Wainaina pia kinajiri miezi minne pekee baada ya serikali ya kaunti ya Lamu kumpoteza Naibu Gavana, Raphael Munyua Ndung’u.

Bw Munyua,46, alifariki Septemba 6,2024 wakati akipokea matibabu katika chumba cha matibabu ya dharura (CCU) kwenye hospitali ya Nairobi.

Hadi sasa, kaunti ya Lamu imesalia bila Naibu Gavana baada ya juhudi za Gavana Issa Timamy kumteua Waziri wa Kilimo na Usalama wa Chakula, Bw James Gichu, kujaza pengo lililoachwa wazi na marehemu Munyua kugonga mwamba kufuatia hatua ya madiwani wa Lamu kutupilia mbali uteuzi huo mar mbili.

Marehemu, Bi Wainaina alizaliwa kijiji cha Uziwa, Wadi ya Mkunumbi, Lamu Magharibi mnamo mwaka 1989.

Ni mama wa watoto watatu.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*