Ruto ageuza Nyanza nyumbani – Taifa Leo


RAIS William Ruto anaonekena kugeuza Nyanza kuwa nyumbani kutokana na kulitembelea eneo hilo kila mara huku ukuruba wake wa kisiasa na Kinara wa Upinzani Raila Odinga ukiendelea kunoga.

Mnamo Ijumaa, Rais Ruto alikuwa katika uwanja wa Raila Odinga Kaunti ya Homa Bay ambapo alihudhuria fainali ya Kombe la Genowa, mashindano yaliyodhaminiwa na Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga.

Rais Ruto alizuru Homa Bay kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2, 2022 baada ya kushinda kura na uchaguzi wake kuhalalishwa na Mahakama ya Juu.

Hata hivyo, ziara hiyo ilisusiwa na wandani wa Bw Odinga akiwemo Gavana Wanga.

Alirejea Homa Bay mnamo Julai 15, 2023 ambapo viongozi wengi wa kaunti hiyo walisusia hafla ya kumkaribisha nyumbani Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Raymond Omollo.

Kiongozi wa nchi amezuru Homa Bay mara zaidi ya saba kwa muda wa miaka miwili ambayo amekuwa mamlakani huku pia akitua Siaya, Migori na Kisumu ambazo ni ngome za Bw Odinga.

Mnamo Februari, wakati wa Kongamano la Kimataifa la Uwekezaji la Kaunti ya Homa Bay, Rais Ruto alifika na kusema alialikwa na Bi Wanga.

Alisema hangekosa kuhudhuria mkutano huo ulionuiwa kujadili fursa za maendeleo na uwekezaji katika kaunti hiyo kutokana na umuhimu wake.

Alimrejelea gavana huyo kama mwanamke mwenye ushawishi ambaye nyota yake ya kisiasa ilikuwa ikingáa.

Rais amekuwa katika Homa Bay zaidi ya mara tatu mwaka huu ikiwemo wakati ambapo alihudhuria hafla ya kusherehekea kuteuliwa kwa John Mbadi kama waziri wa fedha.

Mnamo Agosti alizuru Migori, Homa Bay, Siaya na Kisumu kwa siku nne mfululizo akizindua miradi ya serikali.

Mnamo Novemba 26 alipokelewa kishujaa na wakazi wa Kondele baada ya kuhudhuria kongamano moja la kimataifa Kisumu.

Mnamo Januari 2, Rais atakuwa Kaunti ya Siaya ambapo ataungana na Bw Odinga na Rais wa Uganda Yoweri Museveni kufungua uwanja mpya wa Jaramogi Oginga Odinga.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*