RAIS William Ruto anaonekana kuwa na imani na uaminifu katika utendakazi wa Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ndiposa amekuwa akimpa majukumu muhimu kwenye utawala wake.
Jumamosi Desemba 28, 2024, Rais alimteua Bw Mudavadi kuwa kaimu waziri wa habari, teknolojia na uchumi dijitali. Kando na kudumu kama kinara wa mawaziri, Bw Mudavadi pia ni waziri wa masuala ya kigeni.
Gavana wa kwanza wa Kiambu William Kabogo ameteuliwa kuchukua wizara hayo katika mabadiliko yaliyofanywa na Rais Desemba 19. Hata hivyo, bado anasubiri kupigwa msasa na kamati jumuishi ya uteuzi katika bunge la kitaifa na seneti.
Kwenye mabadiliko hayo, aliyekuwa mshikilizi wa wizara hiyo Margaret Nyambura Ndungú aliteuliwa balozi wa Kenya kule Ghana.
Hii si mara ya kwanza Bw Mudavadi anakuwa kaimu waziri. Kabla ya uteuzi wa Kipchumba Murkomen kama Waziri wa Usalama wa Ndani, Bw Mudavadi alikuwa akiisimamia tangu Oktoba 31 baada ya Profesa Kithure Kindiki kuteuliwa kama naibu rais.
Bw Mudavadi angali kaimu waziri wa jinsia baada ya wizara hiyo kuwa wazi tangu Rais ampendekeze Stella Soi Lang’at ambaye uteuzi wake ulikataliwa na Bunge mnamo Julai 2024.
Mnamo Oktoba 5, 2023 Bw Mudavadi aliteuliwa waziri wa masuala ya kigeni baada ya Dkt Alfred Mutua kuhamishiwa ile wizara ya utalii na wanyamapori.
Bw Mudavadi ni kati ya viongozi ambao waliasi kambi ya Raila Odinga kuelekea uchaguzi wa 2022 lakini akahamia mrengo wa Rais Ruto.
Mnamo Agosti 4, 2024 wajumbe wa chama chake cha ANC walipitisha pendekezo la chama hicho kuvunjwa na kujiunga na UDA.
Kwa sasa Rais Ruto amemwani Bw Mudavadi kuvumisha uwanizi wa Bw Odinga katika uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) ambao uchaguzi wake utaandaliwa mnamo Februari mwaka ujao.
Katika mabadiliko mengine yaliyotekelezwa jana, Waziri wa Mazingira Aden Duale atashikilia wizara ya kilimo akisubiri Mutahi Kagwe apigwe msasa na bunge.
Vivyo hivyo, Waziri wa Michezo Salim Mvurya, ambaye alikuwa Waziri wa Biashara kabla ya mabadiliko, atakuwa Kaimu Waziri wa Biashara hadi aliyekuwa Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui apigwe msasa.
Leave a Reply