
MTANDAO wa uzalishaji avokado nchini uko kwenye hatari ya kuporomoka, kufuatia ongezeko kubwa la ada ya cheti cha huduma za usafi wa mimea kinachotozwa wauzaji na wasafirishaji wa matunda hayo nje ya nchi.
Muungano wa Wauzaji wa Avokado Nje ya Nchi (AEAK) unaonya endapo hatua ya taasisi ya Mbegu na Ustawishaji wa Mimea Nchini (Kephis) kuongeza malipo kwa kiwango cha juu haitatathminiwa, huenda sekta ya matunda hayo ikaporomoka.
AEAK, taasisi ya kisheria iliyosajiliwa chini ya Sheria ya Vyama CAP 108 ya sheria za Kenya, inasikitika kuwa ada ya kila kontena linalosafirishwa ng’ambo limeongezwa kutoka Sh1, 500 hadi Sh12, 500.

Kontena moja ya maparachichi linalosafirishwa nje lina uzani wa kati ya kilo 23,000 hadi 24,000, hivyo ongezeko hilo linawakilisha kupanda kwa gharama kwa asilimia 88.
Nyongeza hiyo ya Kephis ilipingwa na AEAK, na baadaye ikasitishwa Julai 2024.
Afisa Mkuu Mtendaji wa AEAK, Joseph Wagurah, amesema malipo hayo yamefufuliwa bila mashauriano ya kina na wadauhusika katika mtandao wa avokado nchini.
“Inasikitisha sana kuwa ada hizi, ambazo zilipingwa na kusitishwa Julai 2024, sasa zinarejeshwa bila mashauriano ya kutosha na wadau wakuu wa sekta,” alisema Bw Wagurah kwenye mahojiano ya kipekee na Akilimali Dijitali.
AEAK inawakilisha zaidi ya wauzaji 200 wa maparachichi nje ya nchi, na inaonya kwamba nyongeza hiyo itaathiri pakubwa sekta hiyo.

“Wauzaji wa avokado wataathirika moja kwa moja kutokana na gharama hii mpya,” Wagurah akatahadharisha.
Wanachama wa AEAK husafirisha nje ya nchi karibu tani 95,000 za maparachichi kila mwaka, mchango unaoingiza takriban Dola za Amerika (USD) milioni 150 kupitia mapato ya fedha za kigeni, kulingana na data ya 2023 ya Wizara ya Kilimo kuhusu mauzo ya ng’ambo ya bidhaa mbichi shambani zinazochukua muda mfupi kukomaa.
“Kabla ya Julai 2024, Kephis ilikuwa ikitoza Ksh1, 500 kwa kila cheti cha Usafi wa Mimea. Kwenye ada mpya, sasa inatoza senti 50 kwa kila kilo na Sh500 kwa cheti kimoja. Hili ni ongezeko la karibu Sh11, 000 (sawa na asilimia 88). Kurejeshwa kwa ada hizi kunahatarisha ukuaji wa sekta hii muhimu na inayostawi,” alionya Bw Wagurah, akitoa wito kwa serikali kuingilia kati.

Muungano wa Wauzaji wa Avokado Nje ya Nchi Kenya linaonya kuwa malipo hayo hayataathiri tu maendeleo yaliyoafikiwa katika uzalishaji wa matunda haya, bali pia yatasababisha mfumko wa gharama ya biashara.
Kilele chake kitakuwa kusitishwa kwa shughuli za usafirishaji wa avokado ng’ambo, jambo ambalo litasababisha upotevu mkubwa wa ajira na kudhoofisha mafanikio yaliyoandikishwa.
“Hivyo basi, tunahimiza kusitishwa mara moja kwa utekelezaji wa ada hizi hadi mashauriano kamili na ya kina na wadauhusika yafanyike, suluhisho kati ya pande zote lipatikane,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa AEAK.
Kwa mujibu wa takwimu za kitabu cha mwaka cha Mamlaka ya Kilimo na Chakula (AFA), eneo linalolimwa maparachichi liliongezeka kutoka hekta 26,561 mwaka wa 2021 hadi hekta 27,807 mwaka wa 2022, huku uzalishaji ukipanda hadi tani 455,279 kutoka tani 432,969 mwaka wa 2021 – hiyo ikiashiria ongezeko la asilimia 5.2.

Wakulima walipata Sh12.6 bilioni mwaka 2022 ikilinganishwa na Sh12.4 bilioni walizopokea 2021.
Barani Afrika, Kenya inaongoza katika uuzaji wa avokado nje ya nchi, kwenye ramani ya dunia ikiorodheshwa kuwa nafasi ya tano bora.
Mexico inaongoza ulimwenguni katika uzalishaji wa avokado.
Leave a Reply