Afueni kwa wafugaji Kenya ikipata masoko mapya ya nyama – Taifa Leo


KIWANGO cha ununuzi wa nyama na bidhaa zake nchini, kinaendelea kuimarika kufuatia kuongezeka kwa masoko.

Hii ni kutokana na kujiunga kwa masoko mapya (mataifa), kwenye mtandao wa masoko ya nyama za Kenya mwaka uliopita.

Masoko hayo mapya ni pamoja na Iran, Ushelisheli, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo yalifunguliwa 2024.

Kulingana na Baraza la Sekta ya Wauzaji wa Nyama na Mifugo Kenya (KEMLEIC), hatua hiyo imesaidia soko la nyama za Kenya kuongezeka kwa asilimia 15.

Kuingia kwa Ushelisheli na DRC – ambazo ni nchi za Kiafrika, KEMLEIC inasema kunadhihirisha uwezo wa bara la Afrika kunogesha soko la nyama na bidhaa zake.

Kuwepo kwa masoko mapya ya nyama ya nje kama vile Iran, Ushelisheli, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo yalifunguliwa 2024, ni afueni kwa wafugaji wa Kenya. PICHA|SAMMY WAWERU

“Afrika ina idadi ya watu zaidi ya bilioni 1.4, na kutokana na ongezeko la mahitaji ya nyama na bidhaa zake, ni dhahiri kuwa tuna masoko ya bidhaa za mifugo,” Afisa Mkuu Mtendaji wa KEMLEIC, Nicholas Ngahu, akaambia Akilimali katika mahojiano.

Ongezeko la idadi ya watu, alisema ni ishara wafugaji Barani Afrika wana soko tayari la bidhaa za mifugo wao.

Kwa pamoja, nchi za Afrika zina Pato la Taifa (GDP) la Dola trilioni 3 (KaribuSh 87.750 trilioni thamani ya Kenya).

Ngahu anasisitiza kuwa Kenya inapaswa kuendelea kutathmini masoko mapya barani Afrika, ili kuboresha sekta ya mifugo, ambayo inawakilishwa pakubwa na maeneo ya jangwani – sehemu kame na nusu-kame (ASAL).

Wakazi katika maeneo haya wanategemea ufugaji kujiendeleza kimaisha na kukithi mahitaji muhimu ya kimsingi.

“Tunapaswa kuendelea kushirikiana na majirani zetu na mataifa mengine Afrika, kwa kuwa nchi nyingi za bara hili hazihitaji leseni za uuzaji au uagizaji wa nyama na bidhaa zake, mradi tu bidhaa zinaafikia viwango vya kimataifa,” Ngahu anasema.

Kampuni za kuuza nyama nje ya nchi kama vile KenMeat kunufaika pakubwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Afisa huyu anabainisha kuwa Kenya ina fursa nyingi za kibiashara katika mtandao wa ufugaji na uuzaji wa nyama.

Masoko ya kiasili ya nyama za Kenya ni nchi za Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia, Kuwait, Oman, na Bahrain.

Nyama na bidhaa zake zinazosafirishwa nje ya Kenya ni pamoja na nyama za ng’ombe, mbuzi, kondoo, na kuku.

Sekta ya Ufugaji inachangia karibu asilimia 12 ya pato la taifa – GDP moja kwa moja na kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Isitoshe, kenye sekta pana ya kilimo inawakilisha asilimia 30 ya mapato.

Kulingana na data za Idara ya Mifugo (2024), chini ya Wizara ya Kilimo na Ustawishaji Mifugo, idadi ya ng’ombe wa maziwa nchini inakadiriwa kuwa milioni 5.1.

Soseji ni kati ya bidhaa za nyama zinazouzwa nje ya nchi. PICHA|SAMMY WAWERU

Kufikia 2023, uzalishaji wa maziwa ulikadiriwa kuwa lita bilioni 5.2 zenye thamani ya Sh312.7 bilioni.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, inaashiria Kenya inajitosheleza kwa uzalishaji wa maziwa.

Idadi ya ng’ombe wa nyama inakadiriwa kuwa milioni 16.3.

Mwaka wa 2023, nchi ilizalisha tani 237,907 za nyama za ng’ombe zenye thamani ya Sh129.5 bilioni.

Mbuzi na kondoo wana mchango mkubwa katika usalama wa chakula na kipato kwa wafugaji, kutokana na uwezo wao kuzaana kwa haraka, kustahimili mazingira magumu na kula aina mbalimbali za malisho.

Soseji zilizopikwa tayari kushabikiwa. PICHA|SAMMY WAWERU

Kenya, inakadiriwa kuwa na mbuzi wapatao milioni 34.9 na kondoo milioni 23.2 ambao walizalisha tani 77,521 za nyama ya mbuzi yenye thamani ya Sh53.9 bilioni na tani 51,691 za nyama ya kondoo yenye thamani ya Sh34.2 bilioni, mtawalia.

Aidha, nchi ilizalisha tani 93,622 za nyama ya kuku kutoka kwa kuku milioni 68.9 zenye thamani ya Sh34.7 bilioni, tani 40,055 za nyama ya nguruwe kutoka kwa nguruwe 840,160 zenye thamani ya Sh19.5 bilioni, na tani 55,204 za nyama ya ngamia kutoka kwa ngamia milioni 4.3 zenye thamani ya Sh32.5 bilioni, miongoni mwa bidhaa nyingine za mifugo.

Kando na nyama, Kenya inajihusisha na biashara kubwa ya mifugo na nchi jirani kwa kununua na kuuza.

Kwa mfano, Kenya huagiza mbuzi kutoka Somalia na kuuza idadi kubwa ya ngamia kwa nchi hiyo.

Kipande cha nyama choma. PICHA|SAMMY WAWERU

Hali kadhalika, Kenya huagiza kondoo kutoka Tanzania na ng’ombe kutoka Uganda na Sudan Kusini.

Mbali na uuzaji wa nyama, bidhaa za nyama, na mifugo, Kenya sasa inasafirisha na kuuza ngozi katika nchi za Afrika Magharibi, zikiwemo Nigeria, Ghana, na Ivory Coast.

Mifugo pia husafirishwa kwenda Misri, Mauritius, na Oman.

Kwa sasa, Kenya ina vichinjio vinane vyenye leseni kuuza nyama na bidhaa zake nje ya nchi.

 



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*