MWEKA Hazina wa Kitaifa wa chama cha ODM Timothy Bosire, kinachoongozwa na aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga, amekataa uteuzi wa Rais William Ruto kuwa mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama (NTSA).
Katika notisi ya gazeti la serikali nambari 391 ya Januari 17, 2025, Rais Ruto alimteua Bw Bosire kuwa Mwenyekiti wa NTSA kwa muda wa miaka mitatu, na kubatilisha uteuzi wa Dkt Manoj Shah.
Jumamosi, Januari 18, Bw Bosire aliambia Taifa Leo kwamba amekataa uteuzi huo.
“Baada ya kushauriana na sehemu ya uongozi, familia yangu na marafiki, nimefikia uamuzi kwamba lazima nikatae uteuzi huu. Ninashukuru aliyeniteua, Mheshimiwa Rais William Ruto,” Bw Bosire alisema.
Bw Bosire anajiunga na orodha ya watu wanaokataa kazi wanazoteuliwa na Rais Ruto wanaotoa sababu mbalimbali.
Aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali Margret Ndung’u hivi majuzi alikataa uteuzi wa Rais Ruto kuwa balozi mpya nchini Ghana.
Kabla ya hatua hiyo ya Dkt Ndung’u, aliyekuwa Mbunge wa Mugirango Magharibi Vincent Kemosi pia alikataa uteuzi huo, akitoa sababu za kibinafsi.
Aliyekuwa mbunge wa Machakos Town Victor Munyaka pia alikataa uteuzi wake kama mwenyekiti wa bodi ya Kenya Animal Genetic Resource Centre.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply