ILIKUWA furaha kwa familia ya Daniel Wanyeki, ambaye alihukumiwa kifungo cha maisha baada ya binti zake wawili kumsingizia unajisi, alipoachiliwa huru baada ya miaka 17.
Wanyeki aliachiliwa huru Jumatano, Desemba 4, 2024 kutoka Gereza Kuu la Kamiti baada ya Mahakama ya Thika kumpa dhamana ikisubiri uamuzi wa iwapo kesi yake itasikilizwa upya endapo Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma atawasilisha ushahidi mpya mahakamani.
Safari yake ya uhuru ilianza 2020 baada ya binti zake kubatilisha ushahidi wao mbele ya Mahakama Kuu ya Kiambu ambayo wiki jana iliamua kwamba anapaswa kusikilizwa upya.
Wanyeki, kupitia wakili wake Kiroko Ndegwa alikuwa amewasilisha ombi katika Mahakama Kuu ya Kiambu asikizwe upya. Mabinti hao waliambia mahakama kwamba walielekezwa na jamaa zao kumsingizia baba yao.
Mahakama ilisema kulikuwa na ushahidi mpya ulihitaji kesi kusikilizwa upya. Ilimuamuru Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma kukusanya ushahidi mpya kuhusu kesi ya Wanyeki.
Alipofikishwa mbele ya Mahakama ya Thika Jumatano ili kusikilizwa upya, Wanyeki kupitia kwa wakili wake Kiroko Ndegwa aliomba kuachiliwa kwa kuwa hakukuwa na ushahidi mpya, ombi ambalo DPP hakupinga.
Hakimu Mkuu wa Thika Stella Atambo alimwachilia kwa dhamana ya Sh100,000 pesa taslimu, na kuamuru DPP awasilishe ushahidi wowote mpya Januari 22, 2025, ana akikosa Wanyeki ataachiliwa huru bila masharti.
Leave a Reply