
KINYUME na vijana wengine ambao hutumia safu za kijamii kujivinjari, kwa mfanyabiashara mchanga Wambui Kiritu ni tofauti.
Mjasiriamali huyu ambaye huoka mikate, keki na vitafunwa, hutumia mitandao ya kijamii kusaka wanunuzi wa bidhaa zake.
Wambui ana upekee kwenye biashara yake, kwani hutumia ndizi zilizoiva kupindukia kama mojawapo ya viungo kuoka snaki.
Kwenye mahojiano na Akilimali, mwasisi huyu wa Bobo Bakes alidokeza kwamba hutumia majukwaa kama X (awali Twitter), Instagram na Tiktok kunogesha soko la bidhaa zake.

“Kila ninapooka mikate, keki na vitafunwa, hupiga picha za kuzipakia kwenye akaunti zangu,” akasema.
Isitoshe, hujirekodi video wakati akiandaa bidhaa na zaidi ya yote kuchangamsha wafuasi wake – ambao pia ni wateja wake wakuu, kwa maigizo.
Wambui alianzisha Bobo Bakes 2020, mwaka ambao Kenya na ulimwengu ilikuwa ikihangaishwa na gonjwa la Covid-19.
Bidhaa zake, aghalabu hulenga familia zenye watoto.
“Hufurahia sana ninapoona watoto wakiridhia bidhaa nilizoandaa,” akasema.
Hutia nakshi keki kwa virembesho, zionekana maridadi ubunifu ambao huvutia wanunuzi na watoto.

Leave a Reply