Arsenal ‘luwere’ EPL baada ya Liverpool kufinya vijana wa Guardiola – Taifa Leo


MANCHESTER, UINGEREZA;

VIONGOZI Liverpool wamejiweka pazuri zaidi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kulipua mabingwa watetezi Manchester City, Jumapili.

Nambari mbili Arsenal walipata pigo baada ya kukubali kichapo cha 1-0 mikononi mwa West Ham, Jumamosi.

Liverpool wamefungua mwanya wa alama 11 juu ya jedwali kupitia mabao ya kipindi cha kwanza kutoka kwa Mohamed Salah na Dominik Szoboszlai ugani Etihad.

Josko Gvardiol (kushoto) wa Man City na Mohamed Salah wa Liverpool wapambana wakati wa mechi hiyo. PICHA | REUTERS

Vijana wa kocha Arne Slot sasa hawajapoteza mechi ya ligi inayosakatwa Jumapili kwa mara ya 14 mfululizo tangu walemewe 1-0 na Crystal Palace mwezi Aprili 2024.

Reds pia waliimarisha rekodi yao ya kupepeta mabingwa watetezi nyumbani na ugenini hadi mechi saba.

Walibwaga City ya Pep Guardiola 2-0 ugani Anfield mwezi Desemba 2024 kabla ya kuwalazimishia dozi sawa na hiyo Jumapili. Reds walidhalilisha hivyo Blackburn Rovers msimu 1995-1996, Manchester United (2000-2001, 2001-2002, 2008-2009 na 2013-2014) na Chelsea (2010-2011).

Ugani Etihad, Szoboszlai alimegea Salah pasi murwa kutokana na kona ya chini ya Alexis Mac Allister iliyokamilishwa kwa ustadi na mvamizi huyo wa Misri dakika ya 14.

Salah alirudisha mkono kwa Szoboszlai aliposuka pasi safi iliyokamilishwa na raia huyo wa Hungary dakika ya 37.

Alexander Isak (kushoto) wa Newcastle na Murillo wa Nottingham Forest wapambana wakati yao uwanjani St James’ Park. PICHA | REUTERS

Katika mechi ya awali Jumapili, Newcastle walifyeka Nottingham Forest 4-3 kupitia mabao mawili ya Alexander Isak ikiwemo penalti, nao Lewis Miley na Jacob Murphy wakaona lango mara moja kila mmoja.

Forest walitangulia kutetemesha nyavu za Newcastle dakika ya sita kupitia kwa Callum Hudson-Odoi kabla ya vijana wa kocha Eddie Howe kuenda mapumzikoni kifua mbele 4-1 baada ya kujaza kimiani mabao yao manne.

Nikola Milenkovic na Ryan Yates walifungia Forest mabao mawili ya mwisho dakika ya 63 na 90, lakini vijana hao wa kocha Nuno Espirito Santo hawakuweza kukamilisha ufufuo.

MATOKEO YA EPL IJUMAA:

Leicester 0-4 Brentford

JUMAMOSI:

Everton 2-2 Manchester United

Bournemouth 0-1 Wolves

Ipswich Town 1-4 Tottenham

Southampton 0-4 Brighton

Arsenal 0-1 West Ham

Fulham 0-2 Crystal Palace

Aston Villa 2-1 Chelsea

JUMAPILI:

Newcastle 4-3 Nottingham Forest

Manchester City 0-2 Liverpool



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*