Arsenal nje Kombe la FA, ‘mashetani wekundu’ Man United wakisherehekea kusonga mbele – Taifa Leo


ARSENAL wamebanduliwa kwenye Kombe la FA na Manchester United kwa mara ya tisa baada ya mashetani wekundu kushinda mipigo ya penalti 5-3 katika mechi ya raundi ya tatu ugani Emirates mnamo Jumapili, Januari 12, 2025.

Vijana wa kocha Ruben Amorim walifunga penalti zao zote kutoka kwa Bruno Fernandes, Amad Diallo, Leny Yoro, Lisandro Martinez na Joshua Zirkzee. Martin Odegaard, Declan Rice na Thomas Partey walitetemesha nyavu za United kutoka kwa kitovi cha penalti, huku ile ya Kai Havertz ikapanguliwa.

Katika muda wa kawaida, Bruno Fernandes aliweka mabingwa watetezi United kifua mbele dakika ya 52 baada ya kukamilisha pasi safi kutoka kwa Alejandro Garnacho.

United, ambao wana mataji 13 ya FA, walipata pigo pale Diogo Dalot alionyeshwa kadi ya pili ya njano dakika ya 61 na kusalia wachezaji 10 uwanjani.

Arsenal inayoshikilia rekodi ya mataji mengi ya Kombe la FA (14) ilisawazisha dakika mbili baadaye kupitia kwa beki Gabriel Magalhaes.

Vijana wa kocha Mikel Arteta walipata fursa ya kuongeza bao la pili dakika ya 72, lakini nahodha Odegaard akapoteza penalti yake iliyopatikana kutokana na kosa na Harry Maguire, ilipopanguliwa na kipa Altay Bayindir. Arsenal itajilaumu yenyewe kwa kutotumia nguvu za mchezaji mmoja kwa karibu saa nzima na pia kutotumia nafasi zao vyema, ingawa kipa wa United pia alisaidia timu yake pakubwa.

Timu zote kutoka Ligi Kuu zilishinda michuano yao Jumamosi isipokuwa West Ham iliyopoteza dhidi ya Aston Villa 2-0 nao Brentford wakaduwazwa 1-0 na Plymouth Argyle.

Liverpool walipepeta Accrington Stanley 4-0, Leicester wakalaza QPR 6-2, Wolves wakauma Bristol City 2-1, Nottingham Forest wakalemea Luton Town 2-0, Chelsea wakanyamazisha Morecambe 5-0, Bournemouth wakachabanga West Brom 5-1, Brighton wakacharaza Norwich City 4-0, nao Manchester City wakabebesha Salford City mabao 8-0.

Jumapili pia haikuwa mbaya kwa timu za Ligi Kuu baada ya Tottenham kukung’uta Tamworth 3-0, Newcastle United kuliza Bromley 3-1, Ipswich Town kukanyaga Bristol Rovers 3-0, Crystal Palace ikazamisha Stockport 1-0 nayo Southampton ikabomoa Swansea 2-0.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*