Baada ya AUC, serikali ielekeze macho yake kwa maendeleo – Taifa Leo


BAADA ya jitihada za serikali ya Kenya kumsakia waziri mkuu wa zamani, Raila Odinga uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kufeli, ni muhimu juhudi sawa na hizo zielekezwe kwa miradi ya maendeleo.

Ingawa nia ya kuimarisha ushawishi wa Kenya katika bara la Afrika kupitia kwa Bw Odinga ni ya kupongezwa, matokeo ya jaribio hili yanasisitiza jambo moja muhimu: yaliyopita si ndwele tugange yajayo.

Kwa hivyo, ni muhimu zaidi kwa serikali ya Kenya Kwanza kusahau jambo hilo na kuanza kuzingatia kwa umakinifu zaidi changamoto zinazolikabili taifa hili.

Hata ingawa serikali italazimika kujizatiti kujivumisha kwa madhumuni ya kushinda uchaguzi mkuu wa 2027 kutokana na uhalisia kwamba upinzani nao haulali, ni muhimu siasa zisiwazubaishe viongozi wetu kiasi cha kufunika mipango ya maendeleo.

Utawala wa sasa lazima uzingatie kubadilisha maisha ya raia wake, hasa katika nyanja za miundomsingi, elimu, huduma za afya, na kuunda nafasi za kazi.

Masuala haya, kinyume na kutafuta sifa za kimataifa, yatakuwa na athari ya moja kwa moja na ya kudumu kwa ustawi wa Kenya.

Kipindi hiki cha kabla ya uchaguzi kinapaswa kuwa wakati wa kutafakari na kushirikiana katika kufanikisha ustawi nchini.

Kuna masuala kadhaa ambayo yanahitaji uangalizi wa haraka wa serikali.

Kwanza, mipango ya kupunguza umaskini. Licha ya maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali, mamilioni ya Wakenya bado wanaishi katika ufukara. Ukosefu wa usawa nao unasalia kuwa donda ndugu.

Hatua za serikali zinazolenga kushughulikia pengo hili zinaweza kubadilisha maisha ikiwa zitatekelezwa ipasavyo.

Zaidi ya hayo, changamoto za miundomsingi Kenya kama vile barabara na upatikanaji wa maji safi, zinahitaji umakinifu wa dhati.

Ukosefu wa ajira kwa vijana kwa sasa ni sawa na janga la kitaifa. Huku idadi kubwa ya watu nchini Kenya wakiwa na umri wa chini ya miaka 35, sharti serikali itoe kipaumbele kwa sera na za kukuza ujuzi, ujasiriamali na kubuni nafasi za ajira kama vile kuanzisha viwanda vipya na kufufua vilivyoanguka.

Kuhusu elimu, zipo changamoto kama ufadhili wa wanafunzi wa vyuo na vyuo vikuu. Mfumo wa sasa ulisitishwa na mahakama hivyo basi kuzua ombwe la ufadhili wa elimu vyuoni. Sharti suala hili lipewe umuhimu.

Katika sekta ya afya, bima mpya imeripotiwa kukumbwa na changamoto tele. Ni muhimu suluhu ipatikane upesi kabla ya vifo zaidi kutokea.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*