KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Tumejaliwa siku hii kubwa na tukufu ili kukumbushana kulihusu neno lake Muumba wetu, Allah (SWT).
Awali ya yote kama ilivyo ada ya dini yetu tukufu ya Kiislamu twaufungua ukurasa wa leo kwa kumwabudu, kumpwekesha, kumshukuru na kumstahi mwingi wa staha Mola wetu. Ni yeye pekee Allah (SWT) anayestahili kuabudiwa kwa kuwa ni yeye pekee ndiye Muumba wa ardhi na mbingu na vyote vilivyomo.
Ama katika ufunguzi uo huo twamtilia dua na kumfanyia kila aina ya maombi Mtume wetu (SAW).
Leo hii ndugu zangu waumini wa dini tukufu ya Kiislamu ni yetu maombi na dua ili pazidi kuwepo amani duniani. Inasikitisha mno kwa namna gani sisi binadamu tupo mbioni kuvumbua kemikali na kuunda silaha kali kali lengo likiwa kuuana na kumalizana.
Bajeti kubwa kubwa za nchi zetu zikitengwa kwa ajili ya silaha na zana za kinyuklia na ulinzi dhidi ya maadui, adui mkubwa akiwa binadamu kwa binadamu.
Sasa hivi dunia imejaa zogo, zahama na kila aina ya vita na vurumai. Lakini Alhamdulillahi tunashukuru kuwa sasa hivi pana afueni na suluhu baina ya Israel na Lebanon. Huu ni mwanzo na mwamko bora na mpya.
Hali hii tunataraji kuona ikisambaa kote duniani. Na hasa katika ukanda wa Gaza. Itafurahisha na kupendeza sana majaaliwa tukiona amani ambayo itaambatana na kusitishwa kwa vita kwenye eneo la Gaza. Mgogoro baina ya Israeli na Wapalestina umeacha athari kubwa na mbaya sana katika ramani ya dunia.
Majuzi, Novemba 29, imeadhimishwa duniani siku ya kimataifa ya kuwakumbuka na kusimama na ndugu zetu Wapalestina. Siku hii imetengwa na imekuwa ikiadhimishwa duniani tangu mwaka 1977. Hadi leo! Na vita vingalipo katika ukanda wa Gaza! Ya Rabi! Binadamu kuuana wenyewe kwa wenyewe.
Takwimu zinaonyesha kuwa kwenye maadhimisho ya mwaka jana, Novemba 29, ndugu zetu wapatao 14,000 walikuwa wametangulia mbele za haki. Allah (SWT) awalaze pema. Nasi atujaalie mwisho mwema.
Mwaka huu imekisiwa ndugu zetu Wapalestina wapatao 53,000 ama kuaga dunia au kutojulikana waliko, 100,000 wakiwa majeruhi, zaidi ya asilimia 60 wakiwa watoto, wanawake na wakongwe.
Maskini binadamu. Hadi lini ya Rabi!
Leave a Reply