Besigye akimbizwa hospitalini baada ya kudhoofika kwa njaa – Taifa Leo


KAMPALA, Uganda

MWANASIASA wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye, ambaye alianza kususia chakula wiki jana, amekimbizwa hospitalini baada ya afya yake kudhoofika, kulingana na runinga moja nchini humo.

Mpinzani huyo wa miaka mingi wa Rais Yoweri Museveni amekuwa akizuiliwa katika gereza moja lenye ulinzi mkali jijini Kampala tangu Novemba mwaka jana.

Besigye “alitekwa nyara” katika taifa jirani la Kenya, ambako alikuwa amezuru kuhudhuria uzinduzi wa kitabu cha mwanasiasa Martha Karua, na kurejeshwa nchini Uganda.

Alishtakiwa katika mahakama moja ya kijeshi kwa makosa mbalimbali, ikiwemo kupatikana na silaha kinyume cha sheria.

Mnamo Jumapili, Serikali ya Uganda iliahidi kuhamisha kesi dhidi ya Besigye hadi katika mahakama ya kiraia huku ikimsihi kuondoa mgomo wake na kurejelea kula.

Lakini mkewe Besigye, Winnie Byanyima alipuuzilia mbali ahadi hiyo akiitaja kama “isiyo ya kweli”.

Besigye, alianza kususia chakula mnamo Februari 10 kupinga kuzuiliwa kwake.

Serikali imeapa kuendelea na kesi ya uhaini dhidi yake katika mahakama ya kijeshi, licha Mahakama ya Juu kuamua kuwa ni kinyume cha Katiba kumshtaki raia katika mahakama hiyo.

Lakini sasa serikali inaonekana kubadilisha msimamo huo kwani inapanga kuhamisha kesi ya Besigye kutoka mahakama ya kijeshi hadi mahakama ya kiraia.

“Kama serikali, tunataka kuheshimu uamuzi wa Mahakama ya Juu,” akasema msemaji wa baraza la mawaziri, na Waziri wa Habari, Chris Baryomunsi, Jumapili.

Awali, kupitia ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X, Waziri huyo alisema kuwa alikuwa amemtembelea Besigye gerezani mnamo Jumapili akiandamana na madaktari wa kiongozi huyo wa upinzani.

“Nilimshauri aondoa mgomo wake na arejelee chakula huku mipango ya kuhamisha kesi yake hadi mahakama ya raia ikiendelea kukamilishwa,” Baryomunsi akaeleza.

Makao Makuu ya Jeshi, ambayo haijatoa kauli yake kuhusiana na tangazo la waziri huyo, awali ilikuwa imepuuzilia mbali uamuzi huo wa mahakama na kusisitiza kuwa kesi dhidi ya Besigye itaendelea katika mahakama ya kijeshi.

Mnamo Ijumaa kiongozi huyo wa chama cha Forum for Democratic Change (FDC) alifika kortini kwa kesi nyingi akionekana mdhoofu zaidi, hali iliyowakasirisha wafuasi wake.

Waziri Baryomunsi alidinda kusema ikiwa ahadi aliyotoa Jumapili ilichochewa na malalamishi kutoka kwa wafuasi wa Besigye.

Mnamo Jumapili Dkt Byanyima alielezea wasiwasi kuhusu hali ya afya ya mumewe huku akishuku uhalali wa ahadi ya serikali kwamba atamhamisha mumewe hadi mahakama ya raia.



Source link

Be the first to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published.


*