HUKU akikabiliwa na shinikizo kali za kisiasa, Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol, Jumanne usiku alitangaza sheria ya kijeshi katika nchi hiyo ya kidemokrasia kwa mara ya kwanza katika karibu miaka 50.
Tangazo lake la usiku wa manane, lililotolewa kwenye televisheni ya taifa saa tano usiku likitaja usalama wa taifa na tishio kutoka Korea Kaskazini, lakini ilikuwa wazi Yoon alichukua hatua hio kali kujibu mfululizo wa shinikizo za kisiasa.
Alisukumwa hadi kufikia hatua ya kutumia sheria ya kijeshi – utawala wa muda wa kijeshi – kama mbinu ya kujikinga na mashambulizi ya kisiasa, wadadisi wanasema.
Lakini tangazo lake lilizua maandamano mara moja nje ya bunge na wabunge walipiga kura ya kukataa hatua hiyo, ambayo walisema haikuwa halali.
Baada ya mashambulizi ya kisiasa ya upinzani, Rais Yoon Jumanne usiku alisema alitangaza sheria ya kijeshi “kuzima vikosi vya kupingana na serikali ambavyo vimekuwa vikileta uharibifu”.
Hilo liliwaweka wanajeshi kuwajibika kwa muda – na kusababisha kutumwa kwa wanajeshi na polisi bungeni ambapo helikopta zilionekana zikitua kwenye paa la Bunge.
Jeshi pia lilitoa amri ya kupiga marufuku maandamano na shughuli za bunge na makundi ya kisiasa, na kuweka vyombo vya habari chini ya udhibiti wa serikali.
Lakini upinzani wa kisiasa wa Korea Kusini mara moja ulitaja tamko la Yoon kuwa kinyume cha sheria na kinyume cha katiba. Kiongozi wa chama cha Yoon mwenyewe, chama cha kihafidhina cha People’s Power Party, pia aliita kitendo chake “hatua mbaya”.
Wakati huo huo, kiongozi mkuu wa upinzani Lee Jae-myung alitoa wito kwa wabunge wake wa Chama cha Democratic kukutana kwenye bunge ili kupiga kura ya kukataa tangazo hilo.
Pia alitoa wito kwa raia wa kawaida wa Korea Kusini kujitokeza bungeni katika maandamano.
“Vifaru, magari ya kubeba silaha na askari wenye bunduki watatawala nchi, Ndugu zanguni, tafadhalini njooni Bungeni.”
Mamia walitii wito huo, wakakimbia kukusanyika nje ya bunge lenye ulinzi mkali. Umati wa waandamanaji uliimba: “Hakuna sheria ya kijeshi! Hakuna sheria ya kijeshi.”
Matangazo ya vyombo vya habari vya ndani ulionyesha baadhi ya makabiliano kati ya waandamanaji na polisi kwenye lango. Lakini licha ya uwepo mkubwa wa kijeshi, mivutano hiyo haikubadilika kuwa ghasia.
Na wabunge pia waliweza kuvukaa vizuizi ili kuingia katika bunge.
Muda mfupi baada ya usiku saa saba usiku saa za Korea, wabunge 190 kati ya 300 wa bunge la Korea Kusini walihudhuria na kulpiga kura ya kupinga hatua hiyo. Tangazo la Rais Yoon la sheria ya kijeshi lilichukuliwa kuwa batili.
Sheria ya kijeshi ni utawala wa muda wa mamlaka ya kijeshi wakati wa dharura, mamlaka ya kiraia inapochukuliwa kuwa haiwezi kufanya kazi.
Mara ya mwisho ilitangazwa nchini Korea Kusini mwaka 1979, wakati dikteta wa muda mrefu wa kijeshi wa nchi hiyo Park Chung-hee alipouawa katika mapinduzi.
Haijawahi kutangazawa tangu nchi hiyo ikumbatie demokrasia ya bunge mnamo 1987.
Lakini Jumanne, Yoon alizua kimbunga hicho, akisema katika hotuba yake ya kitaifa alikuwa akijaribu kuokoa Korea Kusini kutoka kwa “vikosi vinavyopigana na serikali”.
Yoon, ambaye amekuwa na msimamo mkali zaidi kuhusu Korea Kaskazini kuliko watangulizi wake, alitaja upinzani wa kisiasa kama wanaoiunga mkono Korea Kaskazini – bila kutoa ushahidi wowote.
Chini ya sheria ya kijeshi, mamlaka ya ziada hutolewa kwa jeshi na mara nyingi kuna kusimamishwa kwa haki za kiraia na kanuni za sheria na ulinzi.
Yoon alichaguliwa Mei 2022, lakini amekuwa rais asiye na makali
tangu Aprili wakati upinzani uliposhinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu wa nchi hiyo.
Tamko la Yoon liliwashangaza wengi lakini upinzani uliweza kukusanyika haraka bungeni na kuwa na idadi ya kupigia kura kuzima tangazo hilo la sheria ya kijeshi.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA
Leave a Reply