WAZIRI wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, Dkt Andrew Karanja ametetea vikali zoezi la utoaji chanjo kwa mifugo nchini litakaloanza Januari mwaka ujao, 2025, akisema dawa itakayotumika inaundiwa Kenya.
Kinyume na uvumi kwamba shughuli hiyo ina ajenda fiche, Waziri Karanja amesema inalenga kuboresha usalama wa bidhaa za mifugo nchini.
Baadhi ya wakosoaji wa zoezi hilo, wanahoji kuna mataifa ng’ambo yenye ushawishi mifugo wa Kenya kupewa chanjo kwa “nia mbaya.”
Hata hivyo, Waziri wa Kilimo anasisitiza kwamba utoaji huo wa chanjo unalenga kuimarisha usalama wa bidhaa za mifugo; nyama.
Kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya Shirika la Utafiti wa Kilimo na Mifugo Kenya (Kalro), Dkt Karanja aliweka bayana kuhusu mpango huo akisema chanjo itakayotumika inatengenezewa nchini.
“Hakuna chochocte tunachoficha, na ninahakikishia taifa kuwa chanjo itakayotumika imeundiwa Kenya,” Waziri akasema.
Kenya Veterinary Vaccines Production Institute (KEVEVAPI), taasisi ya kiserikali kuunda chanjo za mifugo, Dkt Karanja alisema imekuwa ikitengeneza chanjo dhidi ya Foot and Mouth Disease (FMD) na Peste des petits ruminants (PPR), kwa zaidi ya miaka 12.
Zoezi la kutoa chanjo kwa mifugo wanaolengwa; ng’ombe, mbuzi na kondoo, linatazamiwa kukabiliana na maradhi ya FMD na PPR, ambayo kulingana na Waziri Karanja ni kikwazo kwa Kenya kuuza bidhaa za wanyama hao nje ya nchi.
Alisema chanjo za maradhi hayo kutoka Kenya, zimekuwa zikinunuliwa na mataifa 13 Barani Afrika, ikiwemo nchi jirani ya Uganda.
Alifichua kwamba tayari Uganda imeagiza dozi milioni tatu za chanjo hizo.
“Kando na nchi za Afrika, mataifa yanayounda Milki za Kiarabu (UAE), yamekuwa yakinunua chanjo za FMD na PPR kutoka kwetu (Kenya),” Dkt Karanja alielezea.
Aidha, alisema ni chanjo ambazo zimekuwa zikitumika na kaunti kudhibiti kusambaa kwa maradhi hayo.
“Utoaji chanjo tutakaofanya si jambo geni. Kaunti zimekuwa zikifanya, na zinazokosa zinalemaza oparesheni dhidi ya FMD na PPR, hivyo ni muhimu shughuli hii iwe ya kitaifa na ushirikiano”.
Ng’ombe milioni 21, na kondoo na mbuzi milioni 50 wanalengwa kupewa chanjo kuanzia Januari 2025.
Kando na kuhakikisha kuwa Kenya inawahi soko la ng’ambo la bidhaa za mifugo, Waziri Karanja alisisitiza umuhimu wa wananchi kula nyama ambazo ni salama.
Akizungumza majuzi katika Kaunti ya Wajir, Rais William Ruto alinukuliwa akikosoa vikali wanaopinga chanjo ya mifugo akisema, “Yeyote anayepinga oparesheni dhidi ya ugonjwa wa FMD na PPR ni mwendawazimu, hafikirii au hata ni mjinga”.
Mifugo inatajwa kuwa kati ya visababishi vya athari za mabadiliko ya tabianchi, hususan utoaji wa gesi ya Methane kupitia kinyesi.
Leave a Reply