Rais wa Amerika Donald Trump (kulia) akiwa na Rais wa Israel Benjamin Netanyahu walipokutana awali mwaka jana. Trump ameeleza nia ya Amerika kutwaa Ukanda wa Gaza ili ‘kuleta uthabiti Mashariki ya Kati’. Picha|Reuters
GAZA, PALESTINA
CHINA na Uingereza zimejiunga na mataifa mengine ya Kiarabu kumlaani Rais Donald Trump kutokana na pendekezo lake kuwa Amerika itachukua usimamizi wa ukanda wa Gaza na kustawisha eneo hilo.
Kwenye mkutano na Waziri Mkuu wa Israel Benjami Netanyahu, Rais Trump alisema Wapalestina ambao wameishi Gaza kwa miaka mingi wataondolewa na kuhamishiwa nchi jirani za Kiarabu.
Rais Trump alisema kuwa raia wa Palestina wameumia sana kutokana na vita kati yao na Israel na njia pekee ya kusuluhisha mgogoro huo ni kuwaondoa Gaza.
“Nitastawisha Gaza na kulifanya eneo la kimataifa. Ukanda wa Gaza utakuwa makao mazuri na kila eneo duniani litakuwa na mwakilishi ambaye anaishi Gaza,” akasema Rais Trump.
Netanyahu alimsifu Rais Trump kwa fikira zake nzuri japo maswali yameibuka kuhusu uhalali wa kauli ya rais huyo wa Amerika kisheria.
Raia wengi wa Gaza wana asili ya Wapalestina ambao walitoroka Israel na hawajawahi kurejea makwao kutokana na vita vikali.
Hamas ambalo ni kundi la Wapalestina, lilichukua usukani mwa Gaza mnamo 2007 baada ya wanajeshi wa Israel kujiondoa mnamo 2005.
Hata hivyo, Umoja wa Kimataifa (UN) bado unaona ukanda huo kama mali ya Israel ambayo pamoja na Misri, pekee ndizo zinadhibiti kuingia na kutoka Gaza.
China jana ilisema kuwa Wapalestina wana haki ya kujitawala kwenye ardhi yao na hawatakubali wahamishwe kwa lazima na utawala wa Rais Trump.
“Tunapinga Wapalestina kuondolewa Gaza kwa lazima kwa sababu hiyo ni ardhi yao,” ikasema Wizara ya Masuala ya Kigeni ya China kupitia taarifa.
Uingereza nayo ilisema Wapalestina wanastahili kurejea nyumbani kwao na kuendelea na maisha yao kama kawaida.
“Wanahitaji kusaidiwa na jamii ya kimataifa kwa sababu kwa muda wa miezi 14 ya vita, wamekuwa wakihangaika sana. Hii ndiyo njia pekee ya kupata suluhu kwa vita kati ya Israel na Hamas,” akasema Waziri wa Mazingira wa Uingereza Steve Reed.
Hamas nao waliapa kuwa liwalo na liwe hakuna raia wa Palestina ataondoka Gaza na kusema matamshi ya Rais Trump ni ya kuzua chuki na kusambaratisha makubaliano ya kudumisha amani.
“Hatutaruhusu nchi yeyote ya kigeni kuchukua ardhi yetu au kutudhibiti. Tunatoa wito kwa mataifa wanachama wa Muungano wa Kiarabu na Kiislamu kuandaa mkutano na kutoa taarifa ya kutetea Wapalestina,” ikasema taarifa ya Hamas.
Saudia Arabia nayo ilikuja juu na kusema itakatiza uhusiano wake na Israel iwapo hakutakuwa na jamuhuri ya Palestina. Msimamo huo unaenda kinyume na matamshi ya Rais Trump kuwa Riyadh haikuwa ikitaka Wapalestina wajitawale.
“Tunakataa pendekezo lolote la kuwatoa Wapalestina kwenye ardhi yao na hili si suala la mjadala,” ikasema taarifa kutoka wizara ya masuala ya kigeni ya Saudia, nchi ambayo ina ushawishi mkubwa zaidi kati ya mataifa ya Kiarabu
Leave a Reply